MKUU wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa, amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa uwekezaji mkubwa na wa kimkakati unaoendelea kutekelezwa mkoani humo, hususan kupitia ujenzi wa majengo ya kisasa ya biashara katika eneo la Mutukula pamoja na Kashozi, Manispaa ya Bukoba.
Akizungumza kuhusu uwekezaji huo, Mwasa amesema miradi inayotekelezwa na NHC imekuwa chachu ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Kagera kwa kuimarisha mazingira ya biashara, kuboresha mandhari ya miji na kutoa fursa kwa wananchi kuendesha shughuli zao za kiuchumi katika majengo yenye viwango vya juu na hadhi ya kisasa.
“Manispaa yetu ya Bukoba inaendelea kubadilika kwa kasi, na mabadiliko haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji wa Shirika la Nyumba la Taifa. Majengo yaliyojengwa yanaakisi dhana nzima ya Shirika katika kuwawezesha wananchi kiuchumi pamoja na kuwapatia huduma bora katika mazingira rafiki na salama,” alisema Mwasa.
Aidha, amesisitiza kuwa Mutukula Commercial Complex ni alama muhimu na ya kuvutia kwa Mkoa wa Kagera, hasa ikizingatiwa kuwa eneo hilo ni mpaka wa kimataifa unaopokea wageni wengi wanaoingia na kutoka nchini.
Ameeleza kuwa ubunifu uliotumika katika ujenzi wa jengo hilo umezingatia kikamilifu mahitaji halisi ya wafanyabiashara, ikiwemo miundombinu rafiki inayowawezesha watu wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, kuingia na kutumia jengo hilo kwa urahisi.
Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa Mkoa wa Kagera, Erasto Chilambo, amesema kuwa jengo la Mutukula tayari limepangishwa kwa asilimia 80, hali inayoonesha mahitaji makubwa ya maeneo ya biashara katika eneo hilo.
Hata hivyo, amesema bado zipo nafasi mahsusi kwa ajili ya taasisi za kifedha, hususan benki.
“Hivyo, tunazikaribisha taasisi za fedha kuchangamkia fursa hii adhimu kwa kupanga katika jengo la Mutukula Commercial Complex, ambalo limejengwa kwa viwango vya juu na lipo katika eneo la kimkakati kibiashara,” amesema Chilambo.
Mutukula Commercial Complex ni jengo la ghorofa moja lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa katika eneo la mpaka kati ya Tanzania na Uganda, likiwa na lengo la