Mwenyekiti CCM Kilombero akanusha kuhusika na sauti inayosambaa mitandaoni

0

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilombero, Mkoani Morogoro Mohamed Msuya, amekanusha vikali taarifa inayosambaa mtandaoni ikihusisha sauti inayodai kuwa Chama kinazuia wajumbe wa chama hicho kuuliza maswali katika mkutano mkuu wa chama.

Akizungumza na vyombo vya habari, Msuya alisema, sauti hiyo ni ya kutengenezwa kwa lengo la kumchafua yeye binafsi pamoja na chama chake hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi ambacho kimejaa chuki na fitina zisizo za msingi.

“Clipu hiyo ni ya uzushi mtupu. Ni njama za kunichafua ili nionekane sifai kusimamia uchaguzi wa haki kwani watu wenye nia ovu wameamua kutengeneza sauti na picha kwa malengo yao binafsi,” alisema Msuya.

Alisema, tayari ameliwasilisha suala hilo katika vyombo vya dola kwa ajili ya uchunguzi na kwamba mtu yeyote atakayebainika kuhusika atachukuliwa hatua za kisheria.

Akifafanua zaidi kuhusu madai kuwa hayakutoa nafasi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu kuuliza maswali, Msuya alisema taarifa hizo ni za uongo kwani kila mkutano hufuata utaratibu rasmi wa chama ambao unatoa nafasi kwa wajumbe kuuliza na kupata majibu.

“Katika mikutano yote niliyohudhuria tangu nichaguliwe, wajumbe wamekuwa wakipewa nafasi ya kuuliza na kujibiwa. Hili ndilo taratibu na kanuni za chama zinavyosema na taarifa zinazosambazwa ni za kutunga,” alisisitiza.

Mwenyekiti huyo alisema Julai 2, mwaka huu, alipokea simu kutoka kwa mtu ambaye hakumtaja jina, akimueleza kuwa sauti yake inasambaa mitandaoni na ilipofika saa moja jioni, aliona mwenyewe taarifa hizo zikienea, jambo lililomfanya amuhusishe moja kwa moja na aliyejaribu kumjulisha awali.

“Kwa sasa naliachia suala hili mikononi mwa vyombo vya sheria hata hivyo, nawaomba wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla waepuke kuchafuana mitandaoni kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi,” alisema.

Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero limethibitisha kupokea taarifa rasmi kutoka kwa Msuya na kueleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea na tayari wamemuhoji kiongozi huyo na taratibu nyingine za kisheria zinafuata.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here