MTOTO wa miaka 10 Mtemi Ndamo wa Kijiji cha Kakese, Kata ya Kakese, Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi ameuawa, wakati akichunga ng’ombe.
Akiwa katika mkutano wa hadhara Kijiji cha Kakese, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf, amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 24, 2022, wakati mtoto huyo akiwa machungani, ndipo alipokutana na wahalifu hao waliokuwa wanataka kuiba ng’ombe.
“Pengine aliwatambua na wenyewe wakamtambua, kwa hiyo wakaona jambo la kulimaliza hili tukio ni kufanya ukatili kwa kiumbe kile,”amesema na kuongeza kuwa ng’ombe wamepatikana na watuhumiwa wa mauaji wamepatikana, lakini hakuwataja majina.
Alitoa pole kwa familia iliyokumbwa na kadhia hiyo, huku akiwaahidi wananchi kuwa serikali itaimarisha ulinzi na wote wanaovunja sheria hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.