Na Igamanywa Laiton
GAZETI la ‘New York Time’ la Mei 4, 1963 katika ukurasa wa mbele lilikuwa na picha kubwa ya rangi nyeusi na nyeupe. Picha hiyo ilimpa wasiwasi mkubwa Rais John F. Kennedy mara baada ya kuiona.
Katibu wa Ikulu ya Marekani Dean Rusk alisikika akisema kuwa, picha hiyo ingelipaka matope Taifa hilo na kuwafurahisha adui za Marekani.
Picha hiyo iliyopigwa na mpiga picha mshindi wa tuzo ya Pultzer, Bill Hudson. Ilipata umaarufu kwa muda mfupi na kuzungumziwa kila kona, kuanzia mabaraza ya Kongresi hadi katika madarasa ya shule na vyuo.
Picha hiyo ilikuwa ni ya mvulana mweusi, mwembamba, aliyevalia vizuri akiwa mbele ya askari wawili wa kizungu walioshika kamba za mbwa wawili wakubwa aina ya ‘German Shepherd’ waliokuwa wakimshambulia kijana huyo huku meno yao makali yakiwa nje.
Kijana huyo mweusi alionekana akiwa na sura ya taharuki na wasiwasi huku akiwaangalia mbwa hao wenye meno makali bila kufanya chochote na bila msaada wowote.
Kutokea kwa picha hiyo katika magazeti na kushika vichwa vya habari kulikuwa ni ‘Mafanikio’ kwa ‘mipango’ ya mtu mmoja aliyekuwa nyuma ya pazia. Mtu huyo hakuwa maarufu, alikuwa hafahamiki, hata na askari polisi wa kizungu waliokuwa na mikakati ya kunyamazisha harakati za watu weusi.
Mtu huyo alikuwa anaitwa Whyatt Walker. Ni mtu mweusi kutoka mji wa Massachusetts. Alijiunga na Martin Luther King Jr mwaka 1960 katika harakati za kumkomboa mtu mweusi. Wyatt ndiye alikuwa mtengeneza mipango ya harakati zote za mtu mweusi.
Katika kitabu ‘David and Goliath: Underdogs, Misfits,and the Art of Battling Giants’ cha mwandishi Malcolm Gladwell anaandika kuwa, Wyatt Walker alikuwa ‘Nati na boliti. Mfanya mipango na ‘Mkarabataji’ wa Martin Luther Jr. Wyatt ndiye alikuwa mtengeneza ‘propaganda’ nyuma ya pazia.
Wyatt alikuwa kivuli, uwepo wake katika harakati ulikuwa ni wa chini chini, huku akimuachia Luther Jr jukumu la kupambana katika mwanga na yeye kushambulia katika giza. Uwepo wake katika harakati ulikuwa ni wa kificho kiasi hata baadhi ya wanaharakati wa harakati hizo kutomtambua.
Wyatt na Luther Jr walikuwa wamepiga hesabu na kujua kuwa adui ambaye walikuwa wakipambana naye alikuwa mkubwa mara elfu kuliko wao, hivyo bila kufanya mbinu za ziada wasingeweza kuishinda hiyo vita.
Martin Jr na Wyatt walikuwa na wafuasi wasiozidi elfu ishirini na mbili,wafuasi wachache sana ambao wasingeweza kufanya dunia kuwapa jicho na sikio kuona na kusikia juu ya kile walichokuwa wakikipigania.
Toka mwanzo walikuwa wamechagua njia ya kutotumia vurugu kupigania madai yao, ni wazi walikuwa wakijua kuwa inahitajika akili ya juu kushawishi dunia kugeuka na kuona kile walichokuwa wakikipigania.
Wyatt na Luther Jr walikuwa wamejenga mipango yao juu ya ‘kanuni mbili’ ambazo walikuwa wameona kuwa zingewasaidia kupata kile walichokuwa wakihitaji.
Kanuni ya kwanza ilikuwa ni ‘Mshambulie adui yako kwa uchokozi au mkasirishe adui yako mwenye nguvu kiasi atumie nguvu kubwa kukushambulia, kitendo ambacho kitageuza haiba yake ya nje na kuonekana mkatili’.
Kanuni ya pili ambayo ilikuwa hitimisho la matokeo ya kanuni ya kwanza ilikuwa ni ‘Baada ya kushambuliwa na adui yako mwenye nguvu kuhakikisha haurudishi shambulizi lolote kwa adui yako huyo ila simama kama mtu dhaifu na hakikisha hata mmoja wa wafuasi wako harudishi shambulizi lolote.
Uhakika wa ushindi juu ya kanuni hizi mbili ulikuwa ni asilimia mia, kwani Luther Jr na Wyatt walikuwa wemeona kuwa walichokuwa wakihitaji ni ‘Huruma’ ya dunia na kufahamika kwa kile walichokuwa wakikipigania. Jambo linaloweza kuifanya serikali ya Marekani kuinama na kuwapa kile walichokuwa wakikitaka.
Mtihani pekee waliobaki nao ulikuwa ni jinsi ambavyo wangepata wafuasi wengi wa kutosha kutia uhalali wa kile walichokuwa wakikifanyia harakati. Wakiwa na wafuasi wasiozidi 22,000, haingekuwa kazi rahisi kupata huruma ya dunia na kueleweka.
Na pia kwa uchache wa wafuasi isingekuwa rahisi kuichokoza au kufanya vitendo vya kuikasirisha serikali. Hivyo Wyatt akaja na mbinu mbili ili kupata suluhu.
Njia ya kwanza ilikuwa ni kutangaza maandamano kisha inapofika siku ya maandamano, walikuwa wakichelewa makusudi kuyaanza kwa masaa machache mpaka watazamaji au wapita njia wasiohusika ‘Wadadisi’ kujaa katika barabara na viwanja kushangaa maandamano.
Kwa kuwa huwezi kutofautisha kati ya mtu anayeshangaa maandamano na muandamanaji, watu wote waliokuwa katika viwanja na katika barabara walihesabika kama waandamanaji.
Hivyo vyombo vya habari vilishindwa kutofautisha idadi ya washangaa ‘maandamano’ na ‘waandamanaji’. Taarifa ziliripotiwa kuwa waandamanaji maelfu kwa maelfu wameonekana leo mitaani, kumbe wengi wa maelfu hayo walikuwa ni watazamaji wadadisi tu.
Njia ya pili waliyoitumia ilikuwa ni kualika wanafunzi wa shule za elimu ya sekondari, ambao walikuwa wakikusanyika bila hiyana katika viwanja vya maandamano huku wakiimba nyimbo za shime na mabango makubwa mikononi.
Kisha baada ya umati wa washangaaji, wavulana wa shule na waandamanaji kusongamana katika mitaa na viwanja. Serikali ikafanya kile ambacho Wyatt na Luther Jr walikuwa wakikitaka. Polisi wakiwa na silaha na mbwa wakaanza kutumia nguvu kutaka kuyazuia maandamano.
Picha zikapigwa zikionesha vijana wasio na hatia wakishambuliwa na mbwa. Ni katika maandamano hayo ndiko Bill Hudson alipopiga picha ya kijana asiye na hatia akishambuliwa na mbwa wa polisi. Picha iliyoamsha hisia za watu wengi duniani na kuzipa macho na masikio harakati hizo.
Kuamshwa kwa hisia za huruma juu ya harakati za akina Wyatt na Luther Jr kulikuwa ushindi kwao baada ya kutimia kwa matokeo ya kanuni ya kwanza kuwa ‘Mchokoze adui yako mwenye nguvu ili akushambulie na aonekane katili kwa kuwa ameshambulia mtu asiye na hatia kwa kutumia nguvu kubwa. Njia za akina Wyatt na Luther Jr zilifanikiwa kwani baada ya miaka miwili walipata kile walichokuwa wakikipigania.
Kisa cha Wyatt na Luther Jr kinashabiana kwa kiasi kikubwa na visa vya kuibuka kwa maandamano kila uchao, watu mbalimbali wenye maslahi mbalimbali hutumia umati wa watu wasio na hatia na wasiojua kile wanachokifanya katika barabara au viwanja vya maandamano.
Bahati nzuri ya Wyatt na Luther Jr ni kuwa yule mvulana hakudhurika, lakini mambo sivyo ilivyo katika visa vingi kama hivyo. Kwani katika visa vingine makumi na mamia ya watu huuawa na uharibifu mwingine wa mali na miundombinu hutokea. Tuchukue tahadhari!