Mradi wa ‘Samia Housing Scheme’ watangazwa kwenye maonyesho ya madini Geita

0
Domina Rwemanyila Afisa habari Shirika la Nyumba la Taifa NHC akitoa maelezo kuhusu mradi wa Samia Housing Scheme unaojengwa Kawe katika jiji la Dar es Salaam.

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limejipanga kutekeleza mradi wa ‘SAMIA Housing’ Scheme unaotarajia kujenga nyumba zaidi ya 5000 na kuzalisha ajira zaidi ya Elfu Ishirini na Sita.

Hayo yameelezwa na Daniel Kure Afisa Mauzo na Masoko Mwandamizi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa wakati akizungumzia ushiriki wao katika Maonyesho ya Madini yanayoendelea Mkoani Geita ambapo alisema, wataanza na awamu ya kwanza katika Mkoa wa Dar es Salaam na kisha Dodoma.

Afisa huyo alisema, wameshiriki katika maonyesho hayo ili kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mradi huo na hivyo kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kwa wale wote wenye mahitaji ya nyumba waweze kupata kwa wakati.

Alisema, mradi huo umeangalia vipato vya watanzania wote kwa kuangalia madaraja mbalimbali wakiwemo watumishi wa Serikali, sekta binafsi pamoja na wafanyabiashara.

“Mradi huu hadi utakapokamilika katika awamu zote utagharibu Bill 466 na utekelezaji wake utaanzia eneo la Kawe Tanganyika Packers baada ya hapo ndipo utasambaa kwa nchi nzima na tunatarajia tutajenga Nyumba 5000,” alisema Daniel.

Daniel amewataka wananchi wote wanaohitaji nyumba wahakikishe wanatumia fursa hiyo mapema kwani wataanza kuutekeleza kuanzia mwezi wa kumi na baada ya miezi kumi na mbili watakuwa wameukamilisha.

Aidha, Daniel amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika Maonyesho hayo ili waweze kupata taarifa kamili kuhusiana na mradi huo.

“Nyumba zetu zinakuwa ghali kwa sababu tunapewa eneo na Halmashauri eneo ambalo hakuna miundombinu, barabara, maji na umeme hivyo mara nyingi sisi ndiyo  tunagharamia na hivyo kufanya gharama kuongezaka na kuwa kubwa na watanzania wanaona kama gharama kubwa lakini ukizingatia gharama zote hizo unaona kabisa ubora wa nyumba zanyewe na huduma tunayoitia,” alisema Daniel.

Hata hivyo alisema, Shirika la Nyumba la Taifa  NHC katika kutekeleza hiyo miradi linaingia katika mchakato wa kununua Ardhi pamoja na kuweka miundombinu mbalimbali ili kurahisisha huduma zote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here