Mkataba ujenzi wa daraja la Jangwani kusainiwa

0
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kusaini Mkataba wa Ujenzi wa Daraja katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam ambapo mkataba unatarajiwa kusainiwa mwezi huu.

Bashungwa alisema hayo leo Septemba 02, 2024 jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum,

Janeth Elias Mahawanga aliyehoji lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa Daraja la Jangwani kuanzia Magomeni -Jangwani – Fire ili kuondoa adha wanayopata wananchi wakati wa mvua?

“Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imepanga kujenga Daraja katika eneo la Jangwani lenye urefu wa Mita 390 na kimo cha Mita 15 ambapo hivi sasa taratibu za manunuzi zipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wake”, alisema Bashungwa.

Bashungwa alisema, ujenzi wa Daraja la Jangwani utatumia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maendelezo ya Bonde la Mto Msimbazi.

Aidha, Bashungwa aliongeza kuwa, ujenzi wa Daraja la Jangwani utaenda sambamba na zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kupitia mradi wa Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi (DMDP II).

Katika hatua nyingine, Bashungwa alisema, tayari Wizara ya Ujenzi imeanza kupokea fedha kutoka Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo ya awali kwa Wakandarasi ambao walikuwa wakisubiria fedha hizo ili waendelee na utekelezaji wa miradi ya ujenzi ya barabara na madaraja inayoendelea na kuwaahidi Wabunge fedha hizo zitaanza kutolewa mara moja ili kazi ziendelee.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here