Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe
Na James Mwanamyoto – Lushoto
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe amemuelekeza Mkandarasi Namis Cooperate Limited aliyepewa kandarasi ya Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, kuwapatia vijana wazawa na akina mama kazi zote ambazo hazihitaji utaalamu ili kutengeneza ajira zitakazowapatia kipato ambacho kitainua uchumi wao.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo wilayani Lushoto, wakati wa hafla ya kupokea eneo la Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto iliyohudhuriwa na viongozi wa mkoa, viongozi wa wilaya, wananchi wa lushoto, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na watumishi wa Mahakama.
Prof. Shemdoe amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 4.272 kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hiyo ya Wilaya ya Lushoto, ambapo ujenzi wake utawezesha kuwapatia kipato vijana watakaopewa kazi kwenye ujenzi wa jengo hilo la Mahakama ya Wilaya ya Lushoto.
“Mkandarasi ninakuomba huku nikikuelekeza kwamba, kazi zote ambazo hazihitaji expert wapewe vijana wetu wa hapa Lushoto ili tuweze kutengeneza ajira kwa vijana wetu wa hapa Lushoto,” Prof. Shemdoe amesisitiza.
Sanjari na hilo, Prof. amemtaka mkandarasi huyo kukunua bidhaa za ujenzi zinazopatikana wilayani Lushoto ili kuongeza mzunguko wa fedha kwa wakazi wa Wilaya hiyo ya Lushoto.