KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Miji 28 katika miji ya Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha haraka utekelezaji wa mradi.
Amesema hali ya utekelezaji wa mradi inaridhisha lakini bado mkandarasi anapaswa kuongeza nguvu katika ujenzi ikiwamo eneo la mtambo wa kuchuja maji kwani hakuna changamoto yoyote ya eneo hilo.
Mradi huo unatarajia kuzalisha lita Milioni 51 kwa siku, na umefika asilimia 70 ya utekelezaji ukitarajiwa kukamilika Desemba 2025.
Amesisitiza kuwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati hivyo Wizara ya Maji haitakuwa na nafasi ya kuongeza muda wa utekelezaji.
Mradi wa maji wa Miji 28 katika Mji wa Korogwe, Handeni Muheza na Pangani unatumia chanzo cha maji kutoka mto Pangani na ni moja ya hatua muhimu ya utekelezaji wa gridi ya taifa ya maji ambayo inalenga kutumia vyanzo vya uhakika vya maji.