MIAKA MITATU YA RAIS DKT. SAMIA: TANAPA yatekeleza miradi 59 ya kijamii

0
Kamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Juma Kuji, akizungumza alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu mafanikio ya Shirika hilo.

KATIKA kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limefanikiwa kuboresha mahusiano na jamii zilizo jirani na hifadhi za Taifa katika shughuli za uhifadhi na utalii.

Kamishina Mkuu wa Uhifadhi Mussa Kuji akizungumza jijini Dar es Salaam alisema, kupitia mashirikiano hayo zimepatikana faida mbalimbali ikiwemo kuibuliwa na Kutekelezwa kwa Miradi ya Kijamii “Support for Community Initiated Projects” (SCIPs).

Kuji alisema, katika kipindi hicho, miradi 59 ya kijamii yenye thamani ya Shilingi 30,785,819,981 ilitekelezwa ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa 20, mabweni 2, nyumba 7 pacha za walimu, zahanati 12, nyumba pacha za wauguzi 6, miradi ya maji 6, barabara 5 zenye urefu wa Kilomita 76 na bwalo la chakula kwa wanafunzi na ununuzi wa madawati 680.

Alisema, miradi hii imetekelezwa katika Wilaya za Ruangwa, Makete, Mbeya, Mbarali, Mpanda – Halmashauri ya Nsimbo, Uvinza, Kigoma, Muleba, Bariadi, Bunda, Serengeti, Mbulu, Arumeru, Rombo, Longido, Mwanga, Same, Korogwe, Lushoto, Pangani, Kilosa, Kilombero, Kilolo, Lindi na Ngorongoro (tarafa za Loliondo na Sale).

“Ujenzi wa miradi hii umesaidia kupunguza kero kwa jamii na kuongeza usalama wa wanafunzi na kuwaboreshea mazingira ya kujifunzia na kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya sambamba na upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo,” alisema Kuji.

Aidha, Kamishna Kuji alisema miradi hii imesaidia kuimarisha mahusiano mazuri kati ya jamii na hifadhi na kuifanya jamii kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa Maliasili.

Mradi mwingine ambao umetekelezwa na Shirika hilo ni, Miradi ya Uzalishaji Mali (TANAPA Income Generating Projects – TIGPs) ambapo vikundi 138 vimewezeshwa kwa ajili ya ufugaji wa nyuki, uchakataji wa viungo vya chakula na ufugaji.

Alisema, Shilingi Bilioni 2.4 zilitumika kuwezesha miradi ya uzalishaji mali. Pia, Benki za Kijamii za Uhifadhi “Community Conservation Bank” (COCOBA) 159 zilianzishwa kupitia mradi wa REGROW na kupewa fedha mbegu kiasi cha Shilingi 1,453,272,934.

“Miradi hii imesaidia kuongeza wastani wa pato la wananchi katika maeneo husika na kupunguza utegemezi wa Maliasili,” alisema Kuji.

Pia, TANAPA kwa kipindi cha miaka mitatu, wametoa ufadhili wa masomo kwa wananchi kupitia mradi wa REGROW, ambapo wanafunzi 1,051 kutoka vijiji 60 vinavyotekeleza mradi wa REGROW wamepatiwa ufadhili wa masomo wenye thamani ya Shilingi 4,273,315,700 katika vyuo mbalimbali vya kitaaluma hapa nchini. “Ufadhili huu utasaidia kuongeza kiwango cha uelewa kwenye jamii na kuongeza uwezo wa uzalishaji mali kwenye jamii husika”

Vile vile, TANAPA wamewezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi na Utoaji wa Hati za Kimila (Community Customary Right of Occupancy – CCRO’s) TANAPA kwa kushirikiana na Benki ya Ujerumani (KfW) na Shirika lisilo la kiserikali la “Frankfurt Zoological Society – FZS.”

Kupitia mpango huo, vijiji 57 vya wilaya za Serengeti, Morogoro, Kisarawe, Ulanga, Tunduru na Liwale na kutoa hati za kimila 16,243 vimenufaika na kati ya hati hizo, hati 9,874 zilitolewa kwa jamii kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Nyerere, na hati 6,612 zilitolewa kwenye vijiji vilivyo katika wilaya ya Serengeti vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

“Tunaendelea kuandaa hati za kimila kwenye Wilaya za Bunda, Bariadi, Tarime, Meatu, Itilima na Busega. Uandaaji huu wa matumizi bora ya ardhi unasaidia kupunguza migogoro ya kimatumizi kati ya binadamu na wanyamapori kwenye maeneo husika na kuwajengea usalama katika umiliki wa ardhi kwa jamii zinazopakana na hifadhi,” alisema Kamishna Mussa Kuji, wakati wa Mkutano na Wahariri na Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili Hazina.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here