Miaka 61 ya Mapinduzi nchi ina maendeleo makubwa – Dkt. Mwinyi

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amebainisha kuwa katika miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar nchi imeshuhudia hatua kubwa ya maendeleo katika miundombinu mbalimbali ikiwemo elimu, afya, umeme, maji, barabara, teknolojia, madaraja na bandari katika miradi yote hii wahitimu wa Taasisi hii ni miongoni mwa wahandisi ambao waliotoa mchango mkubwa sana kufanikisha maendeleo hayo.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo kwenye mahafali ya 10 ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 21 Disemba 2024.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amewasisitiza wahitimu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, kuitafsiri elimu waliyoipata kwa vitendo badala ya nadharia ili kutoa mchango wao kwa maendeleo ya nchi.

Rais Dkt.Mwinyi alisema Serikali itaendelea kutambua umuhimu wa taasisi hiyo kama chachu ya maendeleo kwa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi katika sekta mbalimbali.

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi alisema kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ni jitihada ya kutafsiri kwa vitendo dhamira ya elimu ya amali na ufundi na kuwapa mbinu wananchi za kujitegemea ikiwa ni hatua muhimu ya ilani ya Chama cha Afro Shirazi iliyokuwa na dira na malengo ya muda mrefu ya kuandaa rasilimali watu kwa kuitumikia nchi na kusukuma mbele maendeleo.

Hatua hiyo inakwenda sawasawa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 – 2025 inayoweka mkazo kwa vijana kupewa elimu ya amali na ufundi ili wajitegemee badala ya kusubiri ajira chache zilizoko katika mfumo wa Serikali.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa tangu kuanza kwa Awamu ya Nane, Serikali imeipatia taasisi hiyo, miradi mikubwa miwili ikiwemo kuwajengea uwezo Vijana Kujiajiri na Kuajirika katika Sekta ya Uchumi wa Buluu pamoja na mafunzo katika sekta ya ufundi na sayansi na teknolojia yenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa ambayo kumalizika kwake kutaimarisha miundombinu ya Taasisi hiyo pamoja na rasilimali watu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here