WAZIRI wa Madini, Anthony Peter Mavunde amezindua rasmi shughuli za ujenzi wa mgodi wa madini ya Kinywe(Graphite).
Mgodi huo unaotekelezwa na kampuni ya Faru Graphite Corporation kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania (hisa 16%) na Black Rock Mining Limited (hisa 84%) ikiwa ni hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya sekta ya madini nchini.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika katika eneo la Mahenge, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro, Mavunde amesema uzinduzi huo ni ishara ya kasi mpya ya uendelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati katika Sekta ya Madini, kutokana na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mradi huu si uchimbaji wa rasilimali pekee, bali ni injini ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa viwanda, biashara, ajira, na ustawi wa jamii katika eneo la Mahenge kwa ujumla” amesema Waziri Mavunde.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mradi wa Mahenge unatarajiwa kugharimu takribani Dola za Marekani Milioni 510 (zaidi ya Trilioni 1.3)na utazalisha ajira zaidi ya 400 wakati wa ujenzi na zaidi ya 900 ajira za kudumu mgodi utakapoanza uzalishaji kamili.
Nje ya mgodi, takribani ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 4,500 zitachochewa kupitia mnyororo wa thamani wa wachuuzi, wakulima, wasambazaji wa bidhaa na watoa huduma.