Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Uzairu Abdul Athumani
MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Uzairu Abdul Athumani amewataka Wakandarasi wote wa Manispaa hii kuhakikisha wanatekeleza Miradi yote ya Ujenzi kwa wakati ikiwemo Barabara, Shule na Vituo vya Afya ili kukidhi haja za Wananchi.
Uzairu ameyasema hayo leo Januari 6, 2026 akiwa katika Kikao Kazi na Wakandarasi wa Manispaa ya Temeke kilichofanyika eneo la Buza akiambatana na Naibu Meya Nuru Cassian.
Uzairu amesema kwamba yupo tayari kukagua Miradi yote ya Ujenzi mara kwa mara ili kufahamu hali ya Utekelezaji wa Miradi hiyo.
”Jukumu letu sisi ni kusimamia kazi, tutaendelea kupita kila mradi uliopewa na Halmashauri, uwe Mradi wa Barabara au Shule ni muhimu sana Miradi ifanyike kwa wakati”, alisema Uzairu.
Aidha, Uzairu amewahimiza Madiwani wa Kata husika kuhakikisha kuwa wanafanya Ukaguzi wa mara kwa mara wa Miradi ya Ujenzi inayoendelea ndani ya Kata zao kwani Madiwani wana haki ya kuhoji kuhusu mwenendo wa Utekelezaji wa Miradi inayoendeshwa ndani ya Kata.
Kwa Upande wake Naibu Meya amewashukuru Wakandarasi pamoja Wadau wote kwa Ushirikiano wanaotoa kuhakikisha kuwa wanaendelea kuwatumikia Wananchi wa Manispaa ya Temeke huku akitoa rai kwa kila mtu kwa nafasi yake kuhakikisha anashikamana na wenzake katika kutimiza majukumu ya Kiserikali.