MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Uzairu Abdul Athuman ameipongeza kampuni ya Group Six Limited inayotekeleza Ujenzi wa Barabara ya Kilimahewa iliyopo Kata ya Toangoma yenye Urefu wa Kilometa 7.8 kwa Gharama ya Bilioni 14.5 kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili DMDP II.
Uzairu ametoa pongezi hizo wakati wa mwendelezo wa Ziara yake ya kutembelea Miradi ya Maendeleo katika Manispaa ya Temeke ambapo leo Januari 9, 2026 ametembelea Miradi mitatu ya Barabara katika Kata ya Toangoma.
“Kwa niaba ya Serikali, kwa niaba ya Halmashauri na kwa niaba ya wananchi na Mhemiwa Mbunge sisi tunakupongeza kwa kukimbizana na miradi hii kuanzia mwezi wa tatu kutakuwa na mvua sasa angalizo la mvua tahadhari ichukuliwe sasahivi,” alisema Uzairu.
Mradi huo wa Ujenzi wa Barabara ulioanza mnamo Mei 15, 2025 umefikia Asilimia 23 huku ukitarajiwa kumalizika Agosti 15, 2026.
Aidha, Meya ametembelea Barabara ya Masaki yenye Urefu wa Kilomita 3.9 inayojengwa kwa Gharama ya Bilioni 10.6 ambapo Ujenzi wake ulianza kutekelezwa Januari 15, 2025 huku ukitarajiwa kumalizika Aprili 14, 2026.
Kwa upande wake Meneja wa Group Six Limited Ovee Mirze ameahidi kukamilisha miradi yote inayotekelezwa na kampuni hiyo kwa wakati uliopangwa.