MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo, amefanya ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa Shule ya Amali Ruvu na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo.
Kwasasa mradi huo upo katika hatua ya skimu na mkandarasi anaendelea na kazi.
Akizungumza katika eneo la mradi, amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Kabla ya ziara hiyo, Mwakamo alifanya kikao kifupi na watumishi wa Shule ya Sekondari Ruvu Station, ambapo walipata fursa ya kuwasilisha changamoto zao.
Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa ni uhamisho wa watumishi, malipo ya likizo, malimbikizo ya mishahara, pamoja na uchakavu wa nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Kimara Misale.
Aidha, Mwakamo aliwahimiza watumishi na wananchi kushiriki kikamilifu katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kuhakikisha wanapata fursa ya kushiriki katika uchaguzi ujao.
Katika ziara hiyo, alijibu swali la Juma Mohamed kuhusu ujenzi wa barabara ya Mlandizi hadi Ruvu Station, ambapo alieleza kuwa tayari mkandarasi amepatikana, na kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 23 itaanza muda wowote.
Hata hivyo, ziara hiyo ilikatishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika Kata ya Ruvu, ambapo Mwakamo alipanga kufanya mkutano wa hadhara na pia kushughulikia malipo ya fidia kwa jamii ya wafugaji wanaopisha ujenzi wa Shule ya Amali ili mradi huo uendelee bila vikwazo.