MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo, amefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo tofauti ya jimbo hilo, kwa lengo la kujionea hatua za utekelezaji
Katika ziara hiyo, Mwakamo alitembelea bweni la watoto wenye mahitaji maalum lililopo Disunyara ambalo tayari limekamilika. Alipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali na kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum.
Aidha, alitoa wito kwa Halmashauri kuhakikisha bweni hilo linaanza kutumika mara moja kwa ajili ya watoto waliokusudiwa, ili liweze kutimiza malengo yake ya msingi.
Mbunge huyo pia alitembelea mradi wa kituo cha mafunzo ya vijana cha IPOSA kilichopo Msongola.
Kituo hicho kinatarajiwa kutoa mafunzo ya stadi mbalimbali kwa vijana waliokosa fursa ya kuendelea na elimu ya kawaida.
Mafunzo yatakayotolewa ni pamoja na ushonaji, ufundi wa simu, mapishi, ufugaji, stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, pamoja na kilimo cha bustani. Hadi sasa, jumla ya vijana 113 tayari wameshajiandikisha katika kituo hicho.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mwakamo alikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo shikizi cha Kigelo kilichopo Kijiji cha Vikuge, unaohusisha ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja ya walimu.
Alieleza kuwa uamuzi wa kuanzisha mradi huo umetokana na changamoto ya wanafunzi kutembea zaidi ya kilomita tatu kufuata elimu, jambo linalowaathiri kwa namna mbalimbali.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Mwakamo alikabidhi jumla ya mabati 170, ambapo mabati 120 yametolewa kwa ajili ya kupaua kituo shikizi cha Kigelo, na mabati 50 kwa ajili ya shule ya msingi Vikuge.
Mbunge huyo ameendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya viongozi wa Serikali, jamii na wadau wa maendeleo katika kuleta maendeleo.