Mbeto: Wananchi hawataki ushahidi wa kipolisi kwa maendeleo ya Z’bar

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM ) kimesema viongozi wa ACT Wazalendo watasubiri sana kupata ushahidi wa kipolisi ili kuona shime ya maendeleo ya Zanzibar ya miaka minne iliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi

Pia, chama hicho kimesisitiza iwapo wananchi na wafuasi wa ACT wanayashuhudia maendeleo kwa macho yao, upotoshaji unaofanywa na viongozi wao hauna maana yoyote

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema maendeleo yalioshamiri Zanzibar chini ya utawala wa Rais Dkt. Mwinyi yanahitaji kuendelezwa.

Mbeto alisema, kwa kazi kubwa ya kiutendaji , utelekezaji na ufanisi wa kisera uliofanyika, Rais Dkt. Mwinyi ana haki ya kuchaguliwa tena kwa mara ya pili akamilishe kazi alioianzisha.

Alisema, wananchi hawahitaji ushahidi au upelelezi wa polisi hadi ukamilike ndipo kesi ya msingi isikilizwe na mahakama, badala yake kila mwananchi ameshuhudia yaliofanywa na Serikali.

“Ushahidi na vielelezo vya ushahidi unahitajika mahakamani. Kuhusu maendeleo ya Zanzibar kila mmoja ni shahidi muaminifu. Mpango wa kubeza kwa mambo yanayoonekana ni jambo lisilokubaliwa na wananchi,” alieleza.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisisitiza wakati Rais Dkt. Mwinyi akikabidhiwa Awamu ya Nane ya utawala na mahali alipoifikisha Zanzibar, kila mmoja angependa kiongozi huyo amalizie kipindi cha pili.

“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake apewe. Awamu ya Nane imetimiza wajibu wa kuitumikia nchi na watu wake. Yanayoonekana leo Zanzibar huko nyuma hayakuwepo,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema viongozi wa ACT Wazalendo, wameshindwa kuwapotosha na kuwatia ujinga wananchi kwa kuwalazimisha wasiamini mambo yanayoonekana kwa macho yao.

“Kuona siku zote ni kuamini. Yaliyotekelezwa na SMZ miaka minne iliyopita yanaonekana. Iweje viongozi wa upinzani wawasemee wananchi wakati kila mtu ana macho akishuhudia mabadiliko?” alihoji Mbeto.

Katika maelezo yake, Mbeto aliongeza kusema kuwa utekelezaji wa sera na ahadi zote zilizo ahidiwa katika kampeni ya kuwania urais mwaka 2020, zimetimizwa ikiwemo na ahadi binafsi za mgombea urais kupitia CCM.

“Rais Dkt. Mwinyi atashinda uchaguzi Oktoba mwaka huu. Kushinda kwake kidemokrasia utakuwa mwanzo wa kung’ara kwa Zanzibar kiuchumi kwa maendeleo yatakayoishangaza Afrika Mashariki,” alisema Mwenezi huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here