Mbeto: Wagombea wanaotoa rushwa wakataliwe mchana kweupe

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wanachama wake kuelewa kuwa wagombea wote wa Udiwani, Uwakilishi na Ubunge watakaotoa rushwa ili wapate nyadhifa hawatapigania maslahi ya umma badala yake watajali maslahi binafsi.

Pia, chama hicho kimewakumbusha wanachama na watendaji dhamana wa CCM, kujua rushwa siku zote itabaki kuwa adui wa haki; inayodhalilisha utu.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, ameeleza hayo na kuwakumbusha wagombea watakaothibitika kutoa rushwa, matokeo ya ushindi wao yatafutwa.

Mbeto alisema, tokea enzi za vyama vya ASP na TANU, baadae CCM, Katiba, Kanuni na ahadi za mwanachama, zimeitaja bayana rushwa ni adui wa haki.

Alisema, kitendo chochote cha kuomba au kutoa na kupokea rushwa ni kinyume na ahadi za mwanachama, pia ni kukiuka kiapo na ahadi za mwanachama CCM hai.

“Wanachama watakao toa rushwa ili kuwaghilibu wajumbe wawachague wakatani bila huruma. Hao wakipata Udiwani, Uwakilishi au Ubunge, watajali maslahi yao binafsi na kutopigania maslahi ya umma,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi akizidi kuwakumbusha wana CCM, aliwataka kuwachagua wagombea wenye sifa za kutetea sera za chama, wenye uwezo wa kutatua shida na changamoto za maendeleo ya wananchi.

“Msikubali kupoteza utu na haki zenu kwa miaka mitano ijayo kwa kupokea rushwa. Wapimeni wagombea wote iwapo wanatosha na wana sifa za uadilifu. Mkiwauzia utu wenu hamtawaona wakija kuwatumikia,” alieleza Mbeto.

Pia, aliwatahadharisha wajumbe kuelewa kuwa vyombo vya dola, vinafuatilia chaguzi za vyama vyote, hivyo atakayebainika akitoa au kupokea rushwa, atakamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Chama chetu hakijawahi kuruhusu wapatikane viongozi watoa rushwa. Kutoa rushwa ili uwe Diwani, Mbunge au Mwakilishi huko ni kuibaka demokrasia na ubazazi wa kisiasa.” alisisitiza Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here