Mbeto: Ukweli ukidhihiri uongo hujitenga

0

Na Mwandishi Wetu, Pemba

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema zama za ushindani wa siasa usiotoa matokeo chanya, tija wala manufaa kwa jamii zimepitwa na wakati, badala yake wananchi wanataka kuona mambo kwa macho na vitendo.

Maneno hayo yamebainishwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alipozungumza na Waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo ya CCM huko Chachani Kisiwani Pemba.

Mbeto yupo Kisiwani Pemba kuhudhuria Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Alisema, kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, toka kizazi kimoja hadi kingine, wananchi wa Zanzibar, wamekuwa wakibadilika polepole huku wakiachana na siasa za kukaririshwa mambo yasio fikirika.

“Zile zama za watu kukaririshwa au kulishwa maneno yenye siasa za sumu, chuki na hasama, zinaelekea kufikia tamati. Kila mtu Zanzibar sasa ameamka, anataka kushuhudia kwa vitendo na kuona kwa macho yake,” alisema Mbeto.

Katibu huyo mwenezi alisema, utawala wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi tokea ashike madaraka, amekuwa kiongozi wa vitendo, asiyeamini katika hadithi za kufikirika zisizoipatia jamii manufaa na matunda ya maendeleo .

“Hatutaki siasa domo mtindi samli kwa mwenye ng’ombe. Wananchi ni werevu wangependa kuona vitendo na kwa macho yao. Simulizi za nikipata nitafanya hazina nafasi . Watu wanataka kuona aliye madarakani anafanya nini na kuonekana” alieleza Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi amewashauri Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari waliofika Pemba kabla au baada ya sherehe za Mapinduzi, waitembelee Pemba na kushuhudia ustawi mpya wa maendeleo.

“Mwaka 2025 ni Mwaka wa kufunguliwa milango ya kiuchumi na ongezeko la kasi ya maendeleo pemba. Utajengwa uwanja wa kisasa wa Ndege Chakechake . Bandari za Mkoani, Wesha na Wete alisisitiza.

Mbeto alisema, kuna ujio wa Wawekezaji wa ndani na nje ambao watajenga Viwanda Vidogo;Vya kati na Vikubwa Unguja na Pemba. SMZ imepania kuimarisha sekta ya Uvuvi kwa kununua meli zitakazofika masafa ya mbali baharini .

Pia, aliwatolea wito wanamichezo Kisiwani Pemba , wakiwemo wanasoka, wanariadha, wachezaji wa mpira wa pete, masumbwi, kuogelea, wasanii wa muziki wa kizazi kipya na taarabu, kuonyesha vipaji vyao na kufikia ngazi za Kimataifa.

“Siku zote ukweli ukidhihiri uongo utajitenga. Vitendo hunena kuliko maneno. Waacheni wapinzani wetu wabeze maendeleo yaliopo huku wananchi wakijionea yote yanayofanyika” alieleza Mwenezi huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here