Mbeto: Rais Dkt. Samia ni kielelezo cha kiongozi Mwanademokrasia Afrika

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeitaja hotuba iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akivunja Bunge la 12, imeleta matumaini mapya, kurudisha ari na kukua kwa haiba ya ustawi wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidemokrasia nchini.

Vile vile, CCM kimekiri Rais Dkt. Samia amefanya juhudi kubwa, akitumia akili, nguvu za kulitumikia Taifa toka alipochukua kijiti kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Magufuli.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameiita hotuba hiyo ni kabambe iliothibisha uwezo alionao na utendaji wenye ufanisi wa serikali yake.

Mbeto alisema, kupanda kwa takwimu za ukuaji uchumi, pato ghafi la Taifa, ukusanyaji mapato ya ndani na deni la Taifa ikiwemo Shilingi ya Tanzania kukua huku mfumuko wa bei ukishuka; hayo ni mafanikio ya kujivunia.

Alisema, mauzo ya bidhaa za uzalishaji wa ndani nje ya nchi, akiba ya fedha za kigeni iliyopo, akiba ya hifadhi ya chakula, juhudi za kupambana na rushwa na dawa za kulevya, vimempa Rais na Serikali yake heshima ya kipekee.

“Kupitishwa kwa idadi ya miswada Bungeni na kuwa sheria. Kuwepo uhuru wa habari, vyama vya siasa kufanya shughuli zake na msikumo wa kupatikana Katiba mpya siku zijazo ni umadhubuti wa serikali yake,” alisema Mbeto.

Kuhusu uhuru wa mawazo, utoaji wa maoni, kusajili vyombo vipya vya habari ili kufanyakazi zao, ni fursa inayohimiza kasi ya uwajibikaji, kutanuka kwa wigo wa demokrasia na utendaji unaoleta tija na ufanisi.

Mbeto aliyataja masuala yote hayo, si aghalab kuyakuta katika baadhi ya nchi duniani hususan barani Afrika, lakini chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia yote yamewezekana .

“Hotuba ya Rais Dkt. Samia amekunjua mbawa za uongozi wake katika azma ya kuliongoza Taifa. Amejipambanua na kuonyesha umakini alionao katika kutumikia Taifa na wananchi wake,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema, hotuba hiyo ya Mkuu huyo wa nchi, imeelezea kwa kina na juhudi mbalimbali za kimaendeleo zilizochukuliwa ikiwemo mikopo, kukua kwa deni la Taifa kutokana kupanda kwa thamani dola.

“Ilikuwa ni hotuba yenye msisimko yenye kila sababu ya kuungwa mkono na watanzania wote. Unapoyatazama maendeleo yaliyostawi nchini kila Mtanzania anakiri Awamu ya Sita imetimiza wajibu wake,” alieleza.

Hata hivyo Mbeto aliitaja fomula ya R-Nne chini ya utawala wa Rais Dkt. Samia imeifanya Serikali yake kuwa ni uongozi Kidemokrasia na kiongozi anayefuata utawala wa sheria na kuenzi haki za binadamu .

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here