Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekanusha madai batili yanayoenezwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan hakutoka nje ili ajadiliwe kugombea Urais na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.
CCM kimesisitiza, propaganda zinazofanywa na Balozi wa zamani Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, na wenzake ameziita ni utoto na upuuzi mtupu.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameitaja hoja hiyo ni dhamira ya uchochezi usio na maana, imekosa ukweli, mantiki na mashiko.
Mbeto alisema, propaganda iliyofanyika ni kuhaririwa video ambayo ilikuwa ni wakati wa mjadala wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, ndipo Mwenyekiti aliposema ajenda hiyo sio siri, akitaka ijadiliwe hadharani.
Alisema, taratibu zote za kikanuni na kikatiba kwa jumla, zilifuatwa wakati wa ajenda ya uteuzi wa wagombea Urais na kupitishwa wawili hadi tamati ya uamuzi wa Mkutano Mkuu wa Taifa.
“Tunamtambua Polepole toka akiwa Katibu Mwenezi. Laiti chama kisingekuwa makini kimkakati na kimsimamo, alipania kuviza haiba na ustawi wa demokrasia ndani na nje ya chama,” alisema Mbeto.
Pia, alisema Polepole akiwa Mwenezi, alijibebesha majukumu na madaraka kinyume na katiba ya chama, hata kufikia kuingilia na kufanyakazi za Katibu Mkuu wa CCM.
Mbeto alisema, si kweli kama Mwenyekiti aligoma kutoka nje ya mkutano ili ajadiliwe na wajumbe kama inavyodaiwa, badala yake muda wa ajenda ulipowadia alimkabidhi kiti Makamu Mwenyekiti wake Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Mbeto aliongeza kusema, hata uamuzi wa Polepole wa kutaka kufundisha madarasa ya siasa, itikadi na uongozi, mambo hayo hakuwa katika ufahamu wake, kwani kutoa elimu ya siasa ya chama, itikadi, uongozi na maadili si jambo lelemama.
Alisema, baada ya Polepole kuletwa na Mwenyekiti wa CCM Marehemu Rais Dkt. John Magufuli toka mahali alipokuwa, alidhani angepata mwanya wa kufanya atakavyo bila kuhojiwa.
“Tulimshutukia mapema na tulipobaini anayofanya hayana afya kwa mustakabali wa chama tulimkanya. Aliingia CCM kwa vitisho, ubabe na mbwembwe. Tukasema siku za mwanachama huyu kiburi zitahesabika,” alisema Mbeto.
Mwenezi huyo alisema, kila mwanachama alikuwa macho ili asikiteke nyara chama na kwamba CCM kimejengwa kitaasisi, si mradi binafsi wala kampuni, hivyo Polepole muda wote hakufurukuta.
“Hakupita katika Chuo cha chama au kupata Mafunzo nje ya Nchi. Si kada, si mwalimu, si mkufunzi. Hujaijua siasa ya chama, sera na Itikadi yake. Kwa muktadha huo Polepole hakutosha kufundisha wenzake,” alieleza Mbeto.
Alisema, kabla hajawa Katibu Mwenezi CCM, hawakupata kumjua kama mwanachama wake, lakini kutokana na sababu za kimauzauza kutokea, akaingia CCM kama mgeni mualikwa.