Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masoud Othman, kuwaeleza Wazanzibari atawafanyia mambo gani ambayo hayajatekelezwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi pia amwache Hayati Maalim Seif Sharif Hamad apumzike.
Aidha, CCM kimetaja kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, kupitia mabadiliko ya kumi ya katiba ya Zanzibar, hakuna chama cha siasa kinachounda Serikali peke yake bila kuvishirikisha vyama vingine.
Akizungumza katika Afisi kuu ya CCM Kisiwandui , Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis amesema, anachodai Othman kuwa Serilali ya Zanzibar ni CCM peke yake anaonyesha kuchanganyikiwa.
Mbeto alisema, inasikitisha kumsikia Kiongozi aliyekuwa akiheshimika toka akiwa Mkurugenzi wa Ofisi ya Mashitaka baadae kuwa Mwanasheria Mkuuu SMZ, akiamua kuwa muongo namba moja Zanzibar.
Alisema, Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar, imeundwa na Vyama vitatu; CCM, ACT Wazalendo na ADA Tadea, hivyo kudai miaka mitano iliyopita ilikuwa ni Serikali ya CCM peke yake, huo ni zaidi ya uongo.
“Othman kama hana maneno ya kuwaeleza Wazanzibari alipumzishe kulitaja jina la Hayati Maalim Seif kila wakati. Aseme lipi jipya atalofanya ambalo Dkt. Mwinyi bado hajatekeleza. Mwambieni asiwe kama kasuku anayekariri maneno hayo kwa hayo,” alisema Mbeto.
Vile ville, Katibu Mwenezi huyo alisema, Othman ndiye Mshauri Namba moja wa Rais Dkt. Mwinyi akiwa Makamo wake wa kwanza wa Rais, hivyo kama kweli ingekuwa hakubaliani na maamuzi ya SMZ, angepinga akiwa ndani ya kikao cha Baraza la Mapinduzi.
“Mipango, mikakati na maamuzi yote ya SMZ hupitishwa na kikao cha Baraza la Mapinduzi. OMO ni Makamo wa Kwanza wa Rais. Angekuwa mpinzani wa sera na mipango ya Serikali angekataa kuidhinisha ndani ya Baraza la Mawaziri,” alisisitiza.
Mbeto alisema, kitendo cha Makamo huyo wa Kwanza wa Rais kusimama hadharani na kudai mipango yote imefanywa na Serikali ya CCM si kweli kwakuwa ACT ni mshirika wa SMZ, hivyo kudai hakikushirikishwa, ni usaliti mpya.
“Mfikishieni salamu OMO ajiamini kusimama kwa kutumia miguu yake na kujenga hoja. Ikiwa kila akisimama analitaja jina la Maalim Seiif anaithibitishia dunia ni Kiongozi dhaifu asiyejiweza kwa lolote,” alieleza Mbeto.