Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekitaka ACT Wazalendo kutoidanganya dunia na kutoa madai kuwa Zanzibar inadai Haki zake.
CCM kimesisitiza, Zanzibar ina uhuru kamili, kila Mzanzibari anapata Haki za kujitawala tokea Januari 12, Mwaka 1964.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo huku akikitaka ACT Wazalendo kuacha kuipotosha jamii na Ulimwengu.
Mbeto alisema, baada ya Miaka 104 Zanzibar ikitawaliwa chini ya Ufalme kwa kushirikiana na Uingereza, chama cha Ukombozi cha Zanzibar ASP, kimefanikiwa kutwaa Madaraka ya Dola na kuanza kujitawala.
Alisema, chini ASP na sasa utawala ukiongozwa na CCM, Zanzibar itabaki kuwa huru, yenye Serikali yake, Mahakama, Bendera, Rais wake, Katiba, Watu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
“Zanzibar haihitaji mbeleko ya Ukombozi mwingine ili ijitawale. Kupitia Mapinduzi Matukufu ya Wazanzibari wameshagomboka. Wako Huru wakijitawala bila kuingiliwa na yeyote Duniani,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu Mwenezi huyo alisema, matokeo ya kuwepo kwa kabrasha la makubaliano ya Muungano kati ya Mataifa huru ya Tanganyika na Zanzibar hatimae nchi hizo ziliungana kwa hiari, katika utaratibu wa kawaida unaofahamika duniani.
“Haukuwa uamuzi wa uchuro au wenye na majuto Zanzibar kuungana na Tanganyika kupata Taifa moja. Imepata Bendera moja na Kiti kimoja Umoja wa Mataifa,” alisema Mbeto.
Akieleza kwa undani alisema, hata ingetokea Mwaka 1963 kwa Serikali ya ZNP na ZPPP ingeamua kuungana na nchi yoyote Afrika, maamuzi hayo yangeheshimika na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa.
Vile vile, Mbeto alisema Zanzibar baada ya Mwaka 1964 si Koloni la nchi yoyote Duniani, ni nchi Huru inayojiamulia mambo yake yenyewe.
“Dunia inaitambua Zanzibar iko huru. Midhali CCM kitaendelea kuaminiwa na Wananchi kupitia Uchaguzi wa kidemokrasia, kitatekeleza matakwa ya kuwa na Taifa moja Tanzania,” alieleza.
Katibu huyo Mwenezi, alimtaka mgombea Urais kwa kofia ya ACT, Othman Masoud Othman, aendelee kunadi Sera za ACT kama zipo ili kipate ridhaa bila kutumia mbinu za kusema uongo majukwaani.