Na Mwandishi Wetu
KUNA baadhi ya Wanasiasa walijimilikisha Majimbo kutokana na kuwahonga wajumbe wa kamati za siasa na matokeo yake wamekuwa hawana michango ya maana Bungeni na wengine kubaki wakisinzia.
Akizungumza ofisi za CCM Kisiwandui, Zanzibar Julai 16, 2025, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Itikadi Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amewataka wajumbe wakiletewa majina matatu kutomuangalia mtu usoni.
Mbeto alisema, kuna baadhi yao walizoea kutenga pesa za hongo kwa wajumbe wa kamati za siasa na matokeo yake kukawa hakuna uwajibikaji.
“Tunawaletea majina matatu, angalieni mtu atakayewaletea maendeleo, kama alikuwepo na hakufanya lolote muwekeni pembeni,” alisema.
Alisema, wajumbe ni wawakilishi wa wananchi na iwapo wakipitisha mtu sababu ya pesa zake na sio utendaji chama kitampigania atachaguliwa mbunge au mwakilishi, “lakini mwisho wa siku hatawatumikia, mtaanza kulalamika.”
“Mtu anahongwa mchele, pesa laki tatu au tano anapita nyumba moja hadi nyingine kumnadi mgombea kisha baada ya uchaguzi anakuja kulalamika, hamuoni jimboni aliyemchagua, nitakupa kahawa utakunywa tutaagana, sitasikiliza malalamiko ya majimboni,” alisema.
Amewataka wajumbe kuitumia vizuri fursa waliyopewa na kuchagua watakaoshughulika na shida zilizopo na sio matumbo yao.
“Wapimeni kwa uzalendo, uwajibikaji na maendeleo waliyoleta sio kwa mikutano ya usiku na chawa waliobeba mabegi ya pesa,” alisema Mbeto.
Alibainisha kuwa, ushindi wa CCM ni lazima kutokana na idadi kubwa ya wanachama tofauti na vyama vingine ukweli unaothibitishwa na idadi kubwa ya watia nia waliojitokeza kuchukua fomu.