Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi kimemtaka Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche na viongozi wenzake, kushughulikia ombwe la uongozi na ukandamizaji demokrasia ndani ya chama chake na kuacha kumhusisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pia, CCM imemuonya Heche ikimtaka kutotafuta mchawi badala yake atambue udikteta haukai nyumba moja na demokrasia.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyemtaka Heche aache kumhusisha Mwenyekiti wa CCM Dkt. Samia katika sakata lao.
Mbeto alisema, CCM hakina maslahi yoyote na mvurugano unaoendelea Chadema, badala yake alimtaka Heche na wenzake, waachane na Siasa za kibabe kwa kuwa hazitowapa manufaa yoyote.
“Heche na wenzake wajitahidi kuleta umoja ndani ya Chadema. Waachane na Siasa korofi na uongozi wa mabavu. Udikteta ni sumu hatari kwa ustawi wa Maendeleo ya Demomrasia. Udikteta ni zaidi ya Saratani,” alisema Mbeto.
Aidha, alimtaka Makamu huyo Mwenyekiti kutumia lugha za kiungwana anapokuwa majukwaani na kila anapojenga hoja aonyeshe kama amekomaa kisiasa kuliko kutoa matamshi yasiyompa heshima katika jamii.
Mbeto alikosoa hatua ya Heche kuishambulia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa huku akimshauri ni vema ajibu hoja zote kwa nguvu ya hoja kutokana na maswali atakayoulizwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vvya ya Siasa.
Mwenezi huyo alimueleza Heche ajiandae kujibu kwa ufasaha kila swali atakaloulizwa atoe maelezo na ufafanuzi, badala ya kutumia Lugha kali yenye vitisho na bwato.
“Mwanasiasa makini habwati hovyo jukwani hadi akatoka kipovu. Husema kwa kituo, ustadi huku akijibu kila hoja bila jazba au kuropoka,” alieleza .
Mbeto aliongeza kusema, chama cha Siasa kisichoheshimu misingi ya demokrasia, chenye uongozi usio na uwazi na kufinya uhuru wa mawazo, chama hicho kitegemee kupoteza dira na mwelekeo .
Katibu huyo Mwenezi alisema, kitendo cha Heche kutoa matamshi ya vitisho dhidi ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hakikuonyesha heshima na ungwana wa kisiasa kwake binafsi na Chadema.
“Heche aache kumtafuta mchawi nje ya Chadema .Chadema kijipime ili kijue kilipojikwaa na kujisahihisha . Wakijifanya kichwa ngumu kitaendelea kukimbiwa kila uchao .Si ajabu kikafa kikiwa mikononi mwa uongozi mpya wa Heche na wenzake,” alisema Katibu huyo Mwenezi.