Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kuendelea kuhimiza Amani, Umoja na Upendo miongoni mwa watanzania na kuwaasa watanzania wakatae kwa namna yoyote mpango wa kulivuruga Taifa lao.
Vile vile chama hicho kimesisitiza kujenga nguvu ya hoja badala kutumia hoja zenye nguvu kwa ajili ya kutaka kuungwa mkono na wananchi.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, ameeleza hayo huku akisema ushindani wa kisiasa nchini usiwe chanzo cha umwagaji damu za watu na kuiweka rehani Amani ya Taifa .
Mbeto alisema, CCM kitaendelea kushawishi wananchi kwa kutumia sera zake, kuelezea mipango , mikakati na programu za maendeleo ili kuwaondolea wananchi kero katika maendeleo ya kisekta na kuwafanya waendelee kuishi kwa usalama na amani .
Alisema, CCM hata siku moja hakitajihusisha na Siasa zinazotishia Umoja na Amani, badala yake kitasimamia misingi ya sera, miongozo pamoja na kuwaunganisha wananchi kuwa wamoja wakati wote.
“Serikali za CCM zitaendelea kuwatumikia wananchi na kuona umuhimu wa kukiunga mkono chama hicho kupitia chaguzi kuu au za serikali za mitaa na kukiweka madarakani kwa hiari. Serikali zetu zitaendelea kuongoza dola kwa matakwa ya wapiga kura si kinyume chake,” alisema Mbeto.
Aidha, alisema chama hicho siku zote kitabaki kikiamini dhana na msingi wa kushika madaraka ni kutumia uchaguzi unaotokana na mtaji wa kura za wananchi si vinginevyo.
“Hatutakataa wala kususia uchaguzi kwakuwa demokrasia ya uchaguzi ndio inayoviweka au kuviondoa vyama vya siasa madarakani. Lazima tuwatumikie watu, kuwahangaikia shida zao na kutatulia kero zinazowakabili katika jamii,” alieleza.
Katibu huyo Mwenezi alisema kazi ya chama cha Siasa makini, si kubeba silaha au kuhubiri uvunjaji wa sheria za nchi. Kazi kubwa ya kila chama ni kujenga ushawishi wa kisera hadi kikubalike ikiwemo kuhimiza amani, utulivu na usalama.
“Kwa miaka sitini sasa watanzania wana imani na CCM pia uhakika wa usalama, utulivu na amani ya Taifa. Wananchi huiunga mkono CCM kwa sera zake, misimamo yake imara na utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” alifafanua Mbeto.
Kadhalika Katibu huyo aliwataka wananchi kuvikataa vyama au viongozi ambao huyatumia majukwaa ya kisiasa kuhubiri shari badala ya kutangaza sera za maendeleo za vyama hivyo.