Na Mwandishi Wetu
WANACHAMA wa chama cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuendelea kujitokeza kukichangia chama cha kupitia mifumo ya kifedha na akaunti zilizofunguliwa kwa ajili kampeni za chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka huu 2025.
Kufanya hivyo kutakifanya chama hicho kufikia lengo lake la wagombea Urais wa chama hicho, Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Mwinyi, Zanzibar kuwafikia takribani watanzania wote nchi nzima, wakati wa kampeni zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Akizungumza na wanahabari Zanzibar, kuhusiana na tathmini ya harambee ya chama hicho Taifa Jiji Dar es Salaam na Hafla ya Chakula cha Usiku ‘Ghala Dinner’ iliyofanyika Zanzibar wiki iliyopita kuchangia chama hicho, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema, uamuzi wa kufanya hivyo umetokana na utashi wa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona haja ya kutoa nafasi kwa kila mwanachama kukichangia chama.
“Awali tulitumia makada kukichangia chama na kutumia pesa zilizotokana na vitega uchumi na ada za kadi lakini mwenyekiti akasema tutoe fursa kila mwanachama achangie chama chake,” alisema Mbeto.
Alibainisha kuwa, fedha zilizopatikana pande zote zitaleta utimamu na kukifanya chama kisifikiri kuhusu pesa wakati ukifika.
Amewataka wanaCCM watumie mifumo waliyoelekezwa kuchangia kwani chama kwa kutumia njia zote za usafiri zikiwemo ‘Chopa’ kufika kila eneo nchini kwa wakati kukingana na ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Licha ya kampeni, mwenezi Mbeto alisema, CCM inajenga jengo kubwa la kisasa la Makao Makuu ya Dodoma likiwa la aina yake kuliko chama kingine chochote cha siasa, Afrika Mashariki na ya Kati.
Pesa za usanifu na ushauri elekezi kwa ajili ya ujenzi huo zimeshalipwa hivyo michango hiyo pia itaelekezwa huko kwani kukingana na idadi ya wanachama zaidi ya Milioni 13 waliopo kila mmoja akitoa Shilingi 10,000 zitapatikana Shilingi Bilioni 13, hivyo ametaka wachangie malengo yafikiwe kwa wakati.