Mbeto azitaka Serikali kutoruhusu siasa kufanyika nyumba za ibada

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimezitaka Serikali zake, kuhakikisha muda wote zinasimamia sheria na kanuni zinazokataza siasa kufanyika ndani ya nyumba za Ibada.

Aidha, chama hicho kimehimiza Serikali, kuhakikisha zinamkabili mtu, watu au kundi lolote linalokusudia kuchanganya dini na siasa.

Ushauri huo umetolewa na Katibu wa NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyevitaka vyombo dhamana vya dola, kusmamia misingi ya haki, uwazi na sheria za nchi.

Mbeto alisema, Tanzania haiwezi kujivunia imefikaje mahali ilipo sasa baada ya miaka zaidi ya sitini kupita, endapo itaachia au kulegeza msimamo wake na kuanza kuruhusu siasa kufanyika ndani ya nyumba za Ibada.

Alisema, ustawi wa amani, utulivu na usalama kwa Tanzania na wananchi wake, umetokana na kutenganishwa imani za dini na siasa.

“Nchi yetu haitasubiri aje Mwalimu mpya kufundisha amani, umoja na utulivu. Hatari ya kuchanganya dini na siasa madhara yake yalijulikana kabla ya Uhuru, kujitawala na Muungano,” alisema Mbeto.

Aliongeza kwa kusema, iwe mwiko na marufuku ya vitu hivyo kuishi nyumba moja na kuhakikisha kila atakayekiuka sheria, taratibu na kanuni, ashikwe sikio haraka.

“Toka au hama katika siasa nenda kwenye nyumba ya Ibada kamtumikie Mungu. Ikiwa shauku yako ni kufanya siasa jiondoe ndani ya nyumba za ibada panda kwenye majukwaa ya siasa,” alisisitiza.

Mbeto alisema, nchi moja jirani kwa kupata uzoefu wa ghasia za kidini, imefuta usajili wa nyumba kadhaa za ibada baada ya kuona kuna viashiria hatarishi.

“Wote wanaotaka kujificha ndani ya nyumba za Ibada huku wakifanya siasa wasionewe aibu. Lazima wafichuliwa, wakatazwe na kufutiwa usajili mara moja,” alisema Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here