Mbeto awataka watanzania kukataa siasa zisizoitakia mema nchi

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka watanzania kutokubali kuzugwa kwa namna yoyote na majaribu ya Siasa za ‘kijinamizi’ zisizoitakia mema nchi yetu zenye zana ya kupoteza ustawi wa Amani na Umoja wa Kitaifa.

Chama hicho pia kimesisitiza na kutaja Amani, Utulivu na Mshikamano uliopo Tanzania kwa miaka sitini, umekuwa ukiwashangaza walimwengu wengi duniani.

Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanziabr , Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyewahimiza Watanzania kuendelea kudumisha Amani, Umoja na Mshikamano wa Kitaifa.

Mbeto alisema, kumekuwa na juhudi za chini kwa chini kwa muda mrefu, zinazofanywa na baadhi ya maadui wa Umoja na Amani ambao wamekuwa wakijaribu kutaka kuwatenganisha watanzania.

Alisema, kuna baadhi ya Wanasiasa na Wanaharakati wamekuwa wakitamani kuliparaganya Taifa kwa kutanguliza maslahi yao binafsi na kutojali maslahi ya Umma.

Aliongeza kusema, watu hao wamekuwa wakifanya majaribu kadhaa ikiwemo kukosoa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wakitumia Ukabila, Ukanda na Udini, lakini kutokana na msimamo imara wa Watanzania, mitazamo yote hiyo batili imejikuta ikigonga mwamba.

“Chama chetu kwa heshima zote kinawaasa na kuwataka wananchi kutofuata mkumbo utakaopoteza Amani na Utulivu. Tunajua kuna vitimbakwiri wachache wanaotumia mgongo wa Demokrasia iliopo ili kutimiza ndoto zao haramu,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema, ni vema Watanzania wakakataa kuzugwa na Wanasiasa ambao wamekuwa wakitoa matamshi yenye kuitia shaka na hofu katika jamii.

“Mataifa mengi hususan Barani Afrika yameshavurugwa na kujikuta yakikumbwa na mapigano ya kijamii yasiyokwisha. Nchi kadhaa zimekuwa zikimwaga damu wenyewe kwa wenyewe. Mataifa mengine hadi hayajarudisha maelewano thabit,” alieleza.

Mbeto alisema, kutokana na utamaduni wa watanzania kuwa waaminifu kwa nchi yao, anaamini hakuna jambo lolote gumu lisilozungumzika, hivyo hapajawa na haja kwa baadhi ya watu kutumia lugha za kibabe na vitisho.

“Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amewahi kutukanya tusigombanie fito wakati wote tunajenga nyumba moja. Maneno haya ya dhahabu hayapaswi kupuuzwa kwani ni nadra kuyasikia,” alisisitiza Mbeto.

Aidha, alisema watanzania wana wajibu wa kuwabaini mapema Wanasiasa wa aina hiyo ambao wamekuwa wakihaha usiku na mchana kutaka kulizamisha Taifa letu kwenye bwawa la matope ya machafuko na mgawanyiko.

“Lazima tuwafichue na kukwepa hila, ukorofi na matamshi yao yenye ishara mbaya katika jamii yetu . Maneno siku zote hunena kuliko vitendo. Tusimame imara kupinga tishio lolote la kutugawa kwa namna yoyote,” alisema Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here