Mbeto awashangaa wanaobeza Tanzania kununua umeme Ethiopia

0

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis amewashangaa watu wanaobeza uamuzi wa Serikali kununua umeme kutoka nchini Ethiopia.

Alisema, umeme huo utakuwa na faida kubwa kwa ajili ya shughuli za bandari ya Tanga ambayo imepanuliwa na kuboreshwa, sambamba na kuendesha viwanda vikubwa vinavyojengwa mkoani humo.

Akizungumza na wanahabari kufuatia kuzuka kwa sintofahamu kuhusiana na uamuzi huo wa Serikali Mbeto alisema, kuna wawekezaji wengi ambao wanajenga viwanda vikubwa Tanga, hivi sasa wanachagiza kuwa na umeme wa viwandani.

Akifafanua zaidi alisema, ni gharama kubwa kutekeleza mradi wa usafirishaji nishati hiyo kutoka Chalinze hadi Tanga na ujenzi wa miundombinu yake ni ghali na itakuchukua muda mrefu.

Alisema, gharama za kununua umeme huo zipo chini kulinganisha na nyumbani Tanzania, kwani nchini Unit moja ni senti 9 ukilinganisha na senti 7 zinazotozwa kwa Unit za umeme huo wa Ethiopia na vizuri zaidi miundombinu ipo tayari nchini Kenya ambayo inauleta umeme hadi katika mpaka wa nchi hizo mbili (Kenya na Tanzania), hivyo kuwa rahisi na gharama nafuu.

Alisema, Megawati 100 zitakazonunuliwa zitasaidia uwekezaji unaofanyika kwenye mikoa hiyo ya Kaskazini, huku akisisitiza si mara ya kwanza kwa Tanzania kununua umeme kutoka nchi jirani na anatoa mfano wa umeme unaonunuliwa kutoka Uganda kwa ajili ya Mkoa wa Kagera.

Pia, Serikali inauza umeme Zambia kwa ajili ya matumizi baadhi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kuna laini kubwa inajengwa Zambia na huenda umeme wa Tanzania ukauzwa pia nchini Afrika Kusini.

“Ni uamuzi sahihi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kununua umeme kutoka huko kwani kuna chagizo kubwa la wawekezaji kupitia kituo cha uwekezaji wametuma maombi ya ujenzi wa viwanda vikubwa mkoani Tanga, kwa hiyo nashangaa sana wanaobeza uamuzi huo na sio jambo geni duniani kwa nchi kununua umeme kwa nyingine,” alisema.

Alibainisha kuwa makubaliano ya nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki na Jumuia ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa nchi yenye umeme wa kutosha kuwauzia jirani zao na hata Marekani wananunua umeme Canada na Mexico kwa ajili ya majimbo yanayopakana na nchi hizo.

Pia, Italia inanunua umeme Uholanzi na kimsingi Tanzania ina umeme wa kutosha na sio kwamba wananunua kwa kuwa haupo wa kutosha la hasha isipokuwa nchi ni kubwa yenye mipaka na nchi zaidi ya tano, hivyo sio rahisi kusafirisha umeme maeneo yote, ndio maana hicho kimefanyika.

“Tuna umeme wa kutosha hivi sasa na ili usafirishe umeme kwa ajili ya viwanda vikubwa ni gharama hivyo tuna shida ya ujenzi wa laini hadi kufika unapohitajika na wala sio kutokuwa na umeme wa kutosha,” alisema na kuongeza kuwa, viwanda vitakavyojengwa Tanga vitasaidia kuongeza mapato, ajira na tozo za Serikali tofauti na wengine wanavyofikiria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here