Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeshangazwa na hatua ya Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba na Msomi mwenzake wa Kenya Prof. Patrick Lumumba wa Kenya kwa kuchomoza na kutafuta umaarufu unaopingana na ukweli wa mambo ulivyo.
Vile vile, chama hicho kimewakumbusha Prof. Lipumba na Prof. Lumumba kutumia elimu zao kwa kuwa wakweli na kuacha ushabiki.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo. Khamis Mbeto Khamis, amemtaka Profesa Lipumba, kuacha janja yake ya kisiasa kwa lengo kuwadanganya Watanzania.
Mbeto alisema, fikra na mawazo ya Mwenyekiti huyo wa CUF ni mfu, mtu aliyechoka kimwili na kisiasa hivyo jamii inapaswa kumtazama, kumsikiliza na kumpuuza.
Alisema, kutaka matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 yafutwe, kisha iundwe Serikali ya Mpito, ni kwenda mchomo kwani Tanzania tayari ina Rais aliyechaguliwa na watu, ameshaapa kwa taratibu za kidemokrasia.
“Profesa Lipumba nafikiri amechakaa kisiasa na kifikra. Ameshagota ukingoni hivyo apumzike awapisha wenzake wakiongoze CUF. Kutaka iundwe Serikali ya Mpito ni ishara ya kutapatapa ili ijitutumue kisiasa,” alisema Mbeto.
Aidha,alisema Mwenyekiti huyo hana haki wala ridhaa ya kuzungumzia dhana ya demokrasia, kwakuwa ndani ya chama chake anakabiliwa na tuhuma ya udikteta na kuwa king’ang’anizi wa madaraka.
“Maelezo ya Profesa Lipumba kutaja Uchaguzi haukuwa huru, wazi na haki ni ulalamishi wa jikoni. Uchaguzi umeendeshwa kisheria, kwa uwazi, haki na kidemokrasia. Kutaka Serikali ya Mpito ni ndoto za Alinacha mchana kweupe,” alieleza.
Mwenezi huyo alisema, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ndio iliomtangaza Rais Dkt. Samia ameshinda Uchaguzi kwa Asilimia 98 baada ya kukamilika kwa njia za wazi na haki.
“Nafikiri Profesa Lipumba ameanza kuzeeka kisiasa .Amefilisika na hatoshi tena kusimama mbele ya wanasiasa wenzake. Amekuwa mgombea wa kudumu wa Urais toka Mwaka 1995 hadi 2020 . Arudi Kijijini kwake Ilorangulu akalime Tumbaku,” alisisitiza.
Hata hivyo, Mbeto akimzungumzia Prof. Lumumba, alimshauri msomi huyo angeweka mkazo wa kuishauri Serikali ya Kenya ambako kumekuwa na siasa za vita nikute kwa muda mrefu sasa.
Alisema, Kenya kumetokea mivutano na tafran za kila aina lakini Prof. Lumumba sauti yake haikusikika hadi kufikia Rais Dkt. William Ruto na aliyekuwa Makamo wake wa Rais Rigath Gachuaga kumfuta kazi.
Mbeto, alisema ingekuwa hekima na busara kwa Prof. Lumumba akashughulika na matatizo ya nchi yake, kuzuka kwa ghasia za waandamanaji na jinsi ya kupata suluhu na muafaka wa ndani ya Kenya.