Mbeto awapa somo muhimu vijana Afrika Mashariki

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Vijana Kanda ya Afrika Mashariki na Kati kuzipenda, kuzilinda na kuziepusha nchi zao kwenye kadhia ya mivutano na mizozo isiyo na ulazima wowote.

Pia, chama hicho kimewahimiza Vijana hao kutofuata mkumbo wa pepo za fitna na ushawishi wenye taswira ya nguvu ya Ukoloni na kuridhia kupoteza uhuru, utu na thamani ya kujitawala.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo huku akiyakemea makundi ya baadhi ya Vijana wa Afrika Mashariki kwa kutojali maslahi ya nchi zao.

Mbeto aliitaja mivutano, mabishano na mizozo si katika njia sahihi ya kufikia utatuzi na mapatano yanayoweza kufanyika masahihisho kabla ya dhamira za wachota Mali na Rasilimali za nchi zao hawajafikia malengo yao.

Alisema, vyombo vya Ulinzi na Usalama katika nchi zote duniani vinakula kiapo cha kulinda mipaka, Usalama wa Mali na raia wake, hivyo si vyema kwa vyombo hivyo vikachokozwa au kujaribiwa.

“Kazi za Vyombo vya dola zimetajwa kisheria na kikatiba za nchi zote, hivyo si rahisi vikakwepa kutii dhamana hizo na kutojilinda lilipotokea tishio la hujuma au vurugu dhidi ya Amani,” alisema Mbeto.

Aidha, aliwaasa Vijana kutojiona si jukumu lao kuyapenda, kuyalinda na kuyatetea Mataifa yao dhidi ya njama zozote, kwani nje ya Afrika Mashariki Vijana hao hawana mahali pa kuishi.

Katibu huyo Mwenezi alisema, Waasisi wa Mataifa hayo wametumia nguvu nyingi, wamepoteza jasho na muda wao hadi baadhi yao kupoteza maisha kwa kupigania Uhuru wa Mataifa hayo kwakuwa kazi ya kuleta uhuru haikuwa nyepesi.

“Bila Vijana kuwa na tahadhari watajikuta wakikwepa kubeba uzalendo hivyo kizazi cha sasa kinaweza kuingia katika historia isio na heshima . Kufuata mkumbo kama bendera inavyofuata upepo si fahari kwao,” alifafanua.

Vile vile, Mwenezi huyo alisema wakoloni hawajawahi kuwa na nia njema na Afrika licha ya kurudi katika nchi zao, kwani mara zote huitamani Afrika na kutaka kuipangia masharti ya hovyo.

“Vijana wa Afrika Mashariki na kati amkeni na kataeni kutumiwa kwa kuzirudisha nyuma kimaendeleo nchi zenu. Babu na bibi zenu mnaowaona leo ni marafiki wema kwenu hawakutaka kuondoka kirahisi na kuiacha huru Afrika,” alisema Mwenezi huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here