Na Mwandishi Wetu
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis, amewataka watanzania kuitunza amani na kuepuka matatizo kama yaliyojitokeza nchini Libya.
Mbeto alizungumza hayo hivi karibuni, kwenye kongamano la amani na kusisitiza kuwa, maendeleo ya nchi yetu yanategemea amani na kutolea mfano wa Libya ilivyoharibika baada ya kutokea machafuko yaliyochochewa na vuguvugu la ‘Arab Spring.’
Vuguvugu hilo la mwaka 2010, lilianzishwa kwa madai ya kupigania mabadiliko katika nchi za Kiarabu katika ukanda wa Afrika kaskazini.
Chimbuko la vuguvugu hilo lilikuwa nchini Tunisia dhidi ya utawala wa Rais Zein el Abidine Ben Ali, na kuvuka mipaka hadi nchi jirani za Misri na Libya na kusababisha viongozi wa nchi hizo Mohamed Housni Mubarak na Muammar Gaddafi kuondolewa madarakani kwa njia zisizo halali.
“Mnashuhudia kulipotokea ‘Arab Spring,’ mnaiona Libya; ilikuwa kila raia analipwa, kijana aliyefikia umri wa kuoa analipiwa mahari na nyumba anapewa, leo Libya ipo wapi?,” alihoji Mbeto.
Mwenezi huyo aliendelea kusema, Libya chini ya utawala wa Gaddafi, ilikuwa na uchumi mkubwa kuliko baadhi ya nchi za Ulaya, lakini baada ya machafuko, nchi hiyo imesambaratika na imeporomoka Kiuchumi.
“Ukienda Benghazi kuna kundi lake, ukija Tripoli kuna kundi lake, jamani wosia wangu, amani, amani amani,” alisisitiza Mbeto.