Mbeto atoa ‘pole’ ACT kubakiwa na viongozi muflisi

0

Na Mwandishi Wetu, Pemba

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesikitishwa na uwezo mdogo wa kisiasa walionao viongozi wa ACT Wazalendo Zanzibar, tokea kilipompoteza aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.

Vile vile, CCM imekitaja ACT kimepungukiwa na viongozi mahiri, wenye uwezo mpana kisiasa, ambapo waliobaki sasa ni wapiga porojo majukwaani.

Ujumbe huo wa ‘pole umetumwa toka CCM na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema, ACT kwa sasa kinaongozwa na Wanasiasa magube na makanjanja.

Mbeto alikitaja chama chochote makini cha Siasa, hutangaza sera zake, kutaja dira na sera zake ili kichaguliwe, badala yake wamebakiwa na viongozi muflisi wanaopiga porojo majukwaani.

Alisema, baada ya viongozi wa ACT kushindwa kuwa wabunifu katika kuendesha siasa za kisasa, wamebaki kulitumia jina Marehemu Maalim Seif huku wakitegemea kupata ushindi wa Urais.

“ACT kimepoteza sifa baada ya kutokea kifo cha Maalim Seif. Hivi sasa kinasubiri majaliwa baada ya kukosa matarajio. Hiyo ni shida kwa chama kutegemea uwezo wa mtu mmoja kukipa chama uhai wa kisiasa,” alisema.

Aliongeza, tofauti iliopo kati ya ACT na CCM ni kwamba, chama chake kina hazina ya viongozi wenye upeo, uzoefu na maarifa ndio maana hata kikifanya mabadiliko ya viongozi hakipati athari zozote.

Kadhalika, Mbeto aliongeza kusema kuwa, ACT kimepoteza idadi kubwa ya Wanasiasa madhubuti ambao walifukuzwa CCM baadae wamekutana na adha na karaha ya mtu anayeitwa Ismail Jussa Ladhu.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema kundi la wanasiasa hodari waliotimuliwa CCM mwaka 1987 miongoni mwao waliandaliwa wakiwa CCM na kukomaa kisiasa.

“Kwa Siasa za uzushi, majungu na fitna mtaalam wake ni Jussa. ACT hakifiki popote akiendelea kuwa kiongozi. Hamad Rashid Mohamed alikorofishana na Maalim Seif kwa njama za Jussa . Jussa ndiye aliyewafitini kina Mohamed Dedes na Juma Duni ili mmoja wapo asigombee Urais,” alisisitiza Mbeto.

Pia, Katibu huyo amewataka Wazanzibari kumchagua tena mgombea wa CCM, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ili akamilishe kazi alioianza ya kuiletea Zanzibar maendeleo.

“Msichoke kwenda na kumsikiliza Ian Smith wa Zanzibar akihubiri siasa za ubaguzi, chuki na hasama. Msikilizeni akipayuka kisha mpuuzeni ili mfanye hamsini zenu,” alisema Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here