Mbeto asisitiza Serikali za CCM kukopa kwa ajili ya Maendeleo

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Serikali zake hazitohofia wala kuacha kukopa kwenye Taasisi za Kimataifa za Fedha na Benki ya Dunia kwa minajili ya kutekeleza shughuli za miradi na ujenzi wa miundombinu.

Pia, chama hicho kimeahidi kitasimamia ahadi na sera za msingi kwa kumaliza changamoto zote zinazowatatiza wananchi mijini na Vijijini.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis ameeeleza hayo mara baada ya kumalizika Baraza la Eid el Fitry lililofanyika kwenye viwanja vya Polisi Ziwani Kisiwani Unguja.

Mbeto alisema, Serikali za CCM ili ziweze kutekeleza ahadi na ilani yake ya uchaguzi kwa ufasaha, zitafanya kila linalowezekana kwa nia ya kuwaletea wananchi wake maendeleo bila kuogopa kukopa.

Alisema, Serikali za CCM hazitacha kutekeleza wajibu wake wa kutumikia wananchi, changamoto za kisekta ikiwemo kuimarisha miradi ya Elimu, Afya, Kilimo, Ufugaji, Uvuvi na kupeleka Maji safi na Salama Vijijini.

Aliongeza kusema ikiwa Mataifa makubwa na tajiri duniani, Marekani, Uingereza, Mataifa yote ya Ulaya, Japan na China, yanakopa ili kusukuma mbele maendeleo ya wananchi wao, Tanzania haina sababu zozote za kuhofia kukopa.

“Hadi sasa deni lote la dunia ni zaidi ya Dola Trilioni 315 yaani mara 3 ya uchumi wa dunia ambao ni takriban dola trilion 105. Kwanini Tanzania iache kukopa kwa ajili ya kusukuma mbele zaidi maendeleo ya watu wake? ” alihoji Mbeto.

Alisema, ikiwa nchi tajiri na zile zinazoendelea zinakopa, Tanzania chini ya Serikali ya CCM, haitaacha kufanya hivyo ili kumaliza changamoto zinazokawiza Maendeleo.

“Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Fedha Duniani (IMF) na zile za Global debt, Marekani, ulaya,China na Japan ndizo nchi zinazoongoza kukopa. Marekani peke yake imebeba asilimia 31.8 ya deni lote la dunia kwenye Mashrika ya dunia na katika sekta binafsi,” alifafanua Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema, CCM hakiwezi kuyumbishwa na Vyama vya upinzani kwakuwa vyama hivyo havina dhamana ya kutumikia wananchi hivyo vinajitahidi kufanya lolote ili kupotosha mambo na kutaka viaminiwe.

Aidha, Mbeto alizisifu Serikali mbili za CCM za Tanzania na Zanzibar kwa kuchukua juhudi, kupanga mikakati na mipango madhubuti kwa azma ya kuitumikia nchi na wananchi wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here