Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimestushwa na baadhi ya taasisi na mashirika ya nje kuhoji kwa vitisho kukamatwa baadhi ya wanasiasa wanaovunja sheria wakati Nelson Mandela wa Afrika Kusini na wenzake walikaa jela miaka 27 bila Mashirika hayo kuhoji.
Pia, chama hicho kimesikitishwa na utamaduni mpya wa Mataifa ya nje kuingilia mambo ya ndani ya serikali za Afrika.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, amesema ikiwa Afrika haiingilii mambo ya ndani ya mataifa mengine, ni makosa Afrika kupangiwa hatma yake na mataifa ya kigeni.
Mbeto alisema, ni lazima na shuruti muhimu kwa Mataifa ya Afrika, kuutafakari mwenendo huo ambao kimsingi, hautoi nafasi kwa serikali za kiafrika kutumia uhuru wake wa kujiamulia mambo yake yenyewe.
Alisema, tabia hiyo inakwenda kinyume na taratibu za msingi, kanuni, miiko ya uadilifu ya diplomasia pia ni ukiukaji mkubwa wa mikataba kimataifa.
“Kudumisha mahusiano na ushirikiano wa Kimataifa ni jukumu litakaloifanya dunia kuwa eneo salama, yanapotumika mabavu na vitisho badala ya kuendeleza mahusiano mema, hayo huwa maonevu ya kifikra na ukoloni Mamboleo,” alisema Mbeto.
Katibu Mwenezi huyo alisema, wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini walipopinga siasa za ubaguzi wa rangi, walifikishwa Mahakamani na kutupwa magerezani kinyume na haki, hakuna nchi yoyote Nje ya Afrika iliyolaani maonevu hayo.
“Wananchi wa Namibia, Msumbiji, Angola, Cape Verde, Zimbabwe na Afrika Kusini walinyanyasika. Hakuna aliyewatetea zaidi ya waAfrika wenzao. Ni ajabu wakandamizaji haki wa zamani wanataka kujikosha ili wajionyeshe kuwa watetezi,” alisema Mwenezi huyo.
Pia, Mbeto alionekana kushangazwa kuona baadhi ya wanasiasa wa upinzani Barani Afrika wakifanya siasa za shari, uvunjaji wa sheria huku wakitegemea kupata nguvu ya utetezi toka kwa Mataifa ya kigeni .
“Lazima Viongozi wa Afrika waanze kujadili kuibuka kwa utamaduni wa kejeli na kuweka azimio na msimamo wa pamoja, haiwezekani watesaji wa zamani, jana na juzi leo wageuke na kuwa watetezi wa haki” alibainisha.
Hata hivyo, Katibu huyo Mwenezi alisema Afrika imepoteza viongozi wake kadhaa kina Patrice Lumumba (DRC) , Abeid Karume (Zanzibar), Thomas Sankara (Bukinafaso), Murtala Mohamed (Nigeria) na Marian Ngwabi (Kongo Brazaville) kwa njama toka nje ya Afrika.