Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi kimelaani matamashi ya Kiongozi Mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe aliyeshangazwa na kujitokeza waandishi wa habari, watangazaji, waigizaji na wachekeshaji kuchukua fomu kuwania Ubunge.
Vile vile, CCM kimemtaka Zitto ambaye ni Mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini, kutambua hata wenye taaluma hizo, nao ni binadamu kama wengine.
Akizumgumza katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Kisiwani Unguja, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameyaita matamshi hayo ya Zitto ni ubaguzi wa wazi.
Mbeto alisema, demokrasia ya uchaguzi haibagui watu kwa rangi zao, kabila, dini au kwa kada zao kitaaluma, badala yake kila mtu ana haki na Uhuru wa kuchagua au kuchaguliwa.
Alisema, wakati Zitto akiwaponda waandishi wa habari, watangazaji, waigizaji na wachekeshaji, Taifa la Ukraine hivi sasa, linaongozwa na Rais ambaye ni mchekeshaji, Volodymyr Zelensky.
Rais huyo, amezaliwa Januari 25, 1978 ni mwanasiasa, mwandishi na mwigizaji wa filamu na mchekeshaji.
“Zitto ametoa matamshi ya dharau, kebehi na dhihaka iliopitiliza dhidi ya taaaluma na fani hizo duniani kote.
Alichokifanya ni unyanyasaji na udhalilishaji mbele ya macho ya dunia,” alisema Mbeto.
Katibu huyo mwenezi alisema, CCM kina wanachama wenye taaluma na fani mbalimbali, hivyo hakitawazuia watu fulani ili kuwaruhusu kundi fulani, wachuke na wengine wazuiwe.
“CCM ni taasisi kubwa ya kisiasa yenye wanachama toka makundi ya watu wenye uelewa, ufahamu, fani na taaluma kadha wa kadha. Istoshe si chama cha kibaguzi iwe wa dini, rangi au asili za watu,” alisema.
Mwenezi Mbeto, alisema imekuwa ada na kawaida ya viongozi wa ACT Wazalendo , mara kadhaa kutumia lugha za kubagua watu kwa asili zao , nasaba na kabila, huku wakikdhani hiyo ndio siasa safi.
“Hakuna makundi ya watu wenye alama na kusema hawa wanafaa kwa Urais, ubunge, udiwani au uwakilishi na wengine wasifae.
Katiba ya nchi inataja usawa kwa binadamu wote mbele ya katiba na sheria,” alibainisha.
Mbeto alimtaka Zitto kusimama hadharani kuwaomba radhi kutokana na matamshi yake hayo ya kibaguzi.