Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuelewa kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba Mwaka huu na Chadema hakitashiriki kwasababu viongozi wake hawakusaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Vile vile, CCM kimemshauri Mnyika awaeleze ukweli wanachama wake kuwa waliokwamisha mchakato wa katiba mpya Mwaka 2014 ni Wabunge wa Chadema na CUF.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis na kusisitiza kuwa, CCM hakijawahi kuwatapeli Watanzania bali waliofanya uharamia wa kukwamisha Katiba mpya ni Chadema na CUF.
Mbeto alisema, isingekuwa Wabunge wa CUF na Chadema kutoka nje ya Bunge Maalum la Katiba, ahadi ya CCM iliyowekwa katika Ilani yake ya Uchaguzi mwaka 2015 -2020, ingeipatia Tanzania Katiba mpya.
Alisema, inashangaza kumsikia Mnyika akieneza uongo na kudai CCM inafanya ulaghai kupitia ilani yake ya mwaka 2025-2030 kwa kuahidi katiba mpya wakati mmoja kati ya waliokwamisha mchakato wa katiba mpya mwaka 2014 ni Mnyika.
“Azma ya CCM iko pale pale ya kupata Katiba mpya ifikapo mwaka 2030. Tuliahidi hivyo Mwaka 2015 na sasa tunasema kwa msisitizo na kumaanisha,” alisema Mbeto.
Katibu huyo mwenezi alisema, miongoni mwa wabunge waliotoka nje Katika Bunge Maalum la Katiba ni Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akiweko Mnyika na Tundu Lissu.
“Mnyika atulize kichwa chake ili aseme kwa kumbukumbu sahihi. CCM hakijawahi kuhofia kuandikwa katiba mpya. CCM wakati wote kinajiamini na kujitegemea kifikra na kiakili” alisema.
Pia, Katibu huyo Mwenezi alisema Rasimu ya katiba ya Tume ya Joseph Warioba ilipendekeza Muungano wa Serikali tatu badala ya mfumo wa Serikali mbili unaotumika sasa
“Bunge Maalum la Katiba na wabunge walio wengi walikataa mfumo huo kwa kuuona ni hatari kwa umoja wa Taifa. Kuunda Serikali tatu ni dhamira ya kuvunja Muungano wenyewe,” alibainisha Mbeto.
Alisema, ukiisoma Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba kwa sehemu kubwa imezingatia madai ya upinzani na kuandikwa mambo mengi mapya ambayo hayakuwepo.
“Kwa kujua kwao kwingi wabunge wa Chadema na CUF wakatoroka Bungeni. Cha ajabu sasa wanaipakazia CCM ndio iliyokataa katiba mpya isipatikane,” alisema Katibu huyo Mwenezi.