Mbeto amtaka Jussa atangaze sera za ACT

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimemtaka Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu kunadi sera za chama chake na sio jina la Hayati Maalim Seif Sharif Hamad kama msingi wa sera.

Hatua hiyo ya CCM imetokana na siku za karibuni chama hicho majukwaani kurejea simulizi zilizopita, hali inayoonyesha hakina sera ya kuwaletea Wazanzibari maendeleo.

“Akae kimya na kuacha kuwapumbaza wananchi kwa siasa za porojo na uchepe,” alisema, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanziabr, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis.

Alimtaka Jussa asilitumie jina la Maalim Seif aliyetangulia mbele ya haki kukinadi chama hicho.

Alisema, kwa wananchi wa Zanzibar hakuna asiyejua kwamba, Jussa alikuwa rafiki mwandani wa Maalim Seif kwa ukuruba na mnasaba wao.

Mbeto alisema, wananchi wanataka kusikia sera za ACT, kisha wazilinganishe na sera zilizoleta maendeleo chini ya Serikali ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

“Kwa Chama cha siasa makini duniani sera huwa ndiyo dira ya ushindani badala ya porojo, kejeli na matusi kama afanyavyo Jussa na wenzake,” alisema Mbeto.

Aidha, alimtaka Jussa asiwafanye Wazanzibari kama watu wasio na macho ya kuona yale yaliyofanyika, au hawajui kutofautisha maendeleo yaliyokuwepo awali na yaliyopo hivi sasa.

Mbeto alimtaka Jussa kuelewa kuwa, Wazanzibari ni watu werevu mno wana akili, maarifa na hekima hivyo hawaghilibiwi kwa porojo na siasa zake za chuki

”Wazanzibari hawako tayari kuendelea kugawanywa kwa siasa za chuki na hasama .Kiu yao ni maendeleo ya nchi yao, Umoja, Usalama na Ustawi wa Amani,” alieleza.

Katibu huyo Mwenezi alimtaja Jussa na wenzake mara nyingi wamekuwa wakihubiri ubaguzi ambao kwa miaka mingi umechangia kuwagawa wananchi wa Unguja na Pemba.

“Maalim Seif hana sifa ya kuitwa shujaa au jemedari wa Zanzibar. Jemedari Mkuu wa Mapinduzi yaliyoleta Zanzibar ukombozi ni Hayati Mzee Abeid Amani Karume kupitia ASP,” alisema Mbeto.

Aliongeza kuwa, Maalim Seif atabaki kuwa kiongozj aliyeheshimika baada ya kupikwa, kuandaliwa kisiasa na kiuongozi toka akiwa mwanachama wa CCM.

Pia, Katibu huyo Mwenezi alimkanya na kumuelimisha Makamu huyo Mwenyekiti wa ACT akimtaka aache kuvuruga historia ya Zanzibar kwa kudai Maalim Seif ni jemedari na shujaa wa Zanzibar.

“Maalim Seif ataheshimika kama Kiongozi aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu, Waziri Kiongozi pia Makamo wa kwanza wa Rais SMZ si vinginevyo,” alisisitiza Mbeto.

Kwa upande mwingine Mbeto alimtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masoud Othman, ajiandae kushindwa katika uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba mwaka huu.

“Jussa huwezi kuzifananisha sifa za uongozi alizokuwanazo Hayati Maalim Seif na Othman. Wazanzibari wanahitaji kupata viongozi wenye maono na wapigania maendeleo hivyo asimlinganishe Othman na Maalim Seif,” alisema.

Kadhalika Mwenezi huyo alisema, Wazanzibari hawawezi kutoa kura zao na kumpigia Othman kwa nafasi ya urais, kwani hata hiyo kazi ya Makamo wa Rais SMZ inaonyesha dhahiri imemshinda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here