Mbeto amtaka Jussa ajiandae kujitwika mzigo wa fedheha Oktoba mwaka huu

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimewataka wanachama wake kumpuuza Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu anayetembea na propaganda kuwa kuna wanaCCM Zanzibar wanaounga mkono upinzani.

Akizungumza Mjini Zanzibar leo 14 Aprili, Katibu Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Mbeto Khamis Mbeto amemtaka Jussa aache tabia za uongo.

Mbeto alisema, CCM kinataka apuuzwe kwani daima amekuwa na silka za kibaguzi zilizojaa uzushi mambo ambayo hakuanza leo.

“Anatapatapa, anajua katika Uchaguzi Mkuu Oktoba kuna aibu kubwa itawapata,” alisema Mwenezi Mbeto.

Alisema, Jussa pia mnafiki na ni mtu wa kujipendekeza kwa maslahi yake binafsi na ndiye kipindi Rais mstaafu Dkt.Amani Karume akiwa madarakani aliyekuwa akitembea na propaganda kuwa ni raia wa Malawi na kumdhihaki kwa kumuita majina ya ajabu.

“Leo kinafiki na tabia yake ya kigeugeu anamsifu Rais huyo mstaafu hadharani na upande mwingine anasambaza uzushi wa kibaguzi kuhusiana na asili ya Rais Dkt.. Hussein Mwinyi,” alisema, Mbeto.

Alibainisha kuwa, uzushi sawa na mfamaji ambaye haishi kutapa tapa kwani ni ndoto upinzani kushinda Zanzibar na asiwe mwongo kuhusu asili ya Rais Dkt. Mwinyi.

“Rais Dkt. Mwinyi amezaliwa Zanzibar, kwao Mangapwani Mkoa wa Kaskazini, Unguja kama yeye Jussa alivyozaliwa Makunduchi Mkoa wa Kusini,” alisema.

Mbeto alisema, jitihada zake za kumbagua Rais Dkt. Mwinyi haziwezi kufanikiwa wala kusikilizwa na watu waungwana wenye akili timamu.

“Karne hii ya 21 ukimuona mwanasiasa anajinasibu kwamba yeye ndiye mwenye asili kuliko wengine ni wa kumwogopa kwani hata babu na bibi yake Jussa walivyoingia Zanzibar kwa ajili ya kazi ya kupeta mpunga na kuuza vyungu inajulikana” alisema Mbeto.

Pia, Katibu huyo Mwenezi aliwataka Wazanzibari kuendelea kumpuuza Jussa kila anapopanda majukwani na kuropoka kwani amekubuhu katika siasa za uzushi, ugombanishi na kubuni mifarakano.

“Wewe Jussa acha kuwataja wanasiasa waliofukuzwa CCM mwaka 1987 ili kujionyesha kama anawajua kuliko watu wengine,” alisema.

Mbeto alisema, hatua ya Makamu huyo Mwenyekiti kutaja majina ya wanachama hao waliofukuzwa CCM mwaka 1987 wakiwa na Maalim Seif Sharif Hamad ni vema pia awaambie kuwa waliondoshwa ili kujenga umoja ndani ya CCM.

Mbeto alisema, Jussa anadanganya pale anaposema hayati Maalim Seif alikuwa akimheshimu sana, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, hayati Sheikh Idrisa Abdul Wakil wakati ndiye Maalim Seif ndiye aliyebabisha hadi Rais huyo akajiuzulu Urais kabla ya muda wake,” alibainisha.

“Jussa kwa hulka na tabia yake ya kujipendekeza, alifanikiwa kumgombanisha Maalim Seif na wanasiasa wenzake kina Hamad Rashid Mohamed, Mussa Haji Kombo, Khatib Hasan Khatib na Mohamed Dedes,” alidai Mbeto,.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here