Mbeto amkanya OMO wa ACT kuacha uchochezi majukwaani

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemkanya mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman kuacha kumhusisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna yoyote na mauaji ya watu.

Kadhalika CCM kimekihimiza chama hicho kiache matamshi yanayowataka Vijana wao wajiandae kufanya fujo ikiwa hakitashinda Uchaguzi.

Maelezo hayo yametolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyemtaka Othman kuacha kutoa hotuba za kichochezi majukwani.

Mbeto alisema, inasikitisha kumsikia Othman mdomo wake ukitoa baridi na moto kwa wakati mmoja, kisha akimtaka Rais Dkt. Samia awalinde wafuasi wa ACT dhidi ya mauaji yoyote.

Alisema, hakuna Mtawala dunia anayelenga kuteketeza wananchi wake “Othman usimhusishe Rais Dk samia na kadhia yoyote ya mauaji. Hakuna mtawala anayeuua raia wake bila hatia. Othman acha maneno ya uchochezi na kumtaka Rais awalinde raia wakorofi na wavunja sheria.”

Katibu huyo Mwenezi alisema, kuna hotuba kadhaa za Othman akisikika kuhamasisha zitokee fujo na ghasia, ambazo zimezihifadhiwa kwa ushahidi wa matamshi yake.

Othman akiwa Gando Mkoa wa Kaskazini Pemba amezungumza na kumtaka Rais Dkt. Samia akiwa awalinde wananchi wa Pemba na mauaji.

”Usiyaweke majina ya Marais Dkt. Samia au Dkt. Hussein Mwinyi katika matukio ya mauaji. Hayupo kiongozi mwenye nia ya kuua raia wake. Wanasiasa tuache kuwatia jazba wananchi na kupandikiza Siasa za chuki,” alieleza.

Aidha, Mbeto aliwaonya vijana wa Zanzibar wakatae kufuata mkumbo kutokana na hotuba zenye jazba zinazotolewa na viongozi wao, kwani wajue kuwa sheria za nchi hazijawahi kulala na kutofanyakazi.

“Binadamu ndio wanaopata usingizi, kulala na kuamka. Sheria Katiba na vyombo vya dola duniani havilali wala kusahau. Atakaekiuka sheria atakamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa ushahidi wa matendo yake,” alisisitiza.

Mbeto hakusita kusema kuwa, wananchi wapenda maendeleo, amani na utulivu, hawataacha kumchagua kwa kura nyingi mgombea wa CCM Rais Dkt. Mwinyi na kumrudisha tena madarakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here