Na Mwandishi Wetu, Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema bado hakijatokea chama cha Siasa makini chenye uwezo na sera za kuzuia ushindi wa CCM katika chaguzi Kuu zote za Tanzania na Zanzibar Oktoba Mwaka huu.
CCM pia kimeahidi kushinda Uchaguzi Mkuu wowote Zanzibar na Tanzania kutokana na ubora wa sera zake, mikakati, oganaizesheni ya chama, Ilani mpya na maandalizi ya nyenzo za kampeni.
Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanziba, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alipohojiwa na waandishi wa habari baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka jiwe la msingi la ujenzi, Makao Makuu ya CCM Jijini hapa.
Mbeto alisema, ushindi wa CCM utatokana na utekelezaji wa sera zake kupitia ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 na kuzinduliwa kwa ilani mpya ya Mwaka 2025 -2030.
Alisema, kazi kubwa ya kukamilisha miradi ya maendeleo iliyofanywa na Marais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, zimefanyika kwa viwango vya juu na kuleta ufanisi wa aina yake.
“Mtaji mkubwa wa ushindi wa CCM, kwanza hutokana na idadi ya wanachama wake Milioni 13 nchi nzima. Utekelezaji wa sera zake na kukamilika miradi ya kimkakati ambayo ni tiketi ya ushindi kwa CCM ” alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, alisema Rais Dkt. Samia, ameliongoza Taifa kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi na maendeleo yanayoonekana, ikiwemo kuacha alama ya kihistoria kujenga jengo la Makao Makuu ya CCM.
Alibainisha kuwa, chini ya uongozi wa CCM na serikali zake, Tanzania imeendelea kujijenga katika siasa za kimataifa kupitia diplomasia yake ya uchumi na kuendeleza ushirikiano wa Kimataifa.
“Maendeleo yanaonekana katika kila kona ya Tanzania na Zanzibar hajawahi kutokea. Kazi ya kutumikia wanachi imefanyika kwa viwango na utekelezaji wa miradi ya kisekta na maendeleo kwa miji na vijijini vyote,” alieleza.
Pia, alisema chini ya uongozi wa Marais hao, Tanzania na Zanzibar zimeendelea kuaminiwa na taasisi mbalimbali za fedha duniani, huku ikipatiwa mikopo iliyosaidia kusukuma mbele maendeleo nchini .
“Kutokana na usimamizi makini wa sera za chama na Ilani Serikali zetu zimetimiza wajibu wake kwa kipindi cha Mwaka 2020 -2025. Mkutano Mkuu wa CCM hapa Dodoma utazindua ilani mpya ya Mwaka 2025-2030. Ni ilani ya maendekeo makubwa yajayo,” alisisitiza Katibu Mwenezi huyo.
Alisema, CCM hakitashindwa Uchaguzi na vyama visivyo na malengo ya sera wala Ilani za uchaguzi. “Kazi ya kujenga chama cha siasa kinachobeba matumaini ya wananchi ni kazi inayohitaji uthubutu, akili na maarifa.”