Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimekitaka ACT Wazalendo kuacha kutunga uongo na kueneza duniani kwa kujifanya hakihusiki kuchochea matukio ya kudhuru watu wakiwemo wanachama wa CCM.
Wanachama hao, wengine wanadaiwa kujeruhiwa vibaya kwa kuwamwagia tindikali, na wengine wamechomewa nyumba zao kwasababu zinazotajwa ni kutokana na tofauti za kisiasa.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis na kumtaka Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa ACT, Othman Masoud Othman kuacha upotoshaji na kulinda heshima yake kutokana na nafasi aliyonayo na elimu yake.
Mbeto alisema, kila Mwananchi na Mkaazi wa Unguja na Pemba, anajua matukio ya kutisha yaliyowaathiri baadhi ya wana CCM yakiwemo matukio ya Mwanajeshi wa JWTZ, KVZ, KMKM, Polisi mmoja kuchinjwa na kuibiwa kwa bunduki moja.
Alisema, matukio hayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na kauli za viongozi wa ACT akiwemo mmoja ambaye aliwahi kutoka hadharani maeneo ya Michenzani na kutangaza huku akiwataka wanachama wao ACT watoke majumbani wakiwa wamebeba silaha za kijadi ili kupigania haki ya chama chao.
Katibu huyo Mwenezi alisema, kuna wana CCM wamejeruhiwa kwenye matukio mbalimbaki akiwemo Khatib Said Khatib, Khamis Hamad Haji, Rashid Massoud Hamad na Raya Khamis Hamad.
Wengine ni Sada Khamis Hamad, Yassir Hemed Abdul, Hassan Khamis Hamad, Ayoub Makame Haji, Juma Khatib Rajab na Abdalla Khamis Mbarouk.
Mbeto alimtaka Mwenyekiti huyo wa ACT anapozumgumzia watu kuathiriwa, awataje watu wote wakiwemo wana CCM kwakuwa pia ni binadamu kama wale wa chama chake ambao huenda si katika matukio ya kweli.
Aidha, alisema kabla ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) kulikuwa na mfululizo wa matukio ya kulipuka kwa mabomu, Viongozi wa Dini, SMZ na watalii kumwagiwa tindikali, lakini baada ya kuwepo SUK matukio hayo hayapo.
“Inasikitisha kumsikia Makamo wa Kwanza wa Rais SMZ akitaja matukio ya watu kuathiriwa na kutoyataja matukio mabaya yaliyowakuta Viongozi wa dini Sheikh Fadhili Soraga aliyemwagiwa tindikali na Padri wa Kanisa Katoliki aliyepigwa risasi na kupoteza maisha,” alieleza Mbeto.
Mbali na hilo, Mbeto alizungumzia upotoshaji unaofanywa na chama hicho, likiwemo suala la kugawana majimbo.
“Othman ameidanganya dunia na kujikosha kinafiki. Si mtu mwenye muamana na si kiongozi Msemakweli. CCM hakijawahi kuwa na mpango na ACT wa kugawana majimbo. Kama ana ushahidi huo auonyeshe hadharani,” alisema Mbeto.
Aidha, alizungumzia madai yaliyotolewa na Othman kwamba kuna watu 4000 wa Jimbo la Gando hawajaandikishwa, ambapo Mbeto alisema watu walioandikishwa jimbo zima la Gando ni 4095 na Mkoa wote wa Kaskazini Pemba ni 148,712.
“Huu ni uongo mpya mweupe wa Othman. Huyu si mtu muaminifu, kwani siku zote hajui kusema kweli. Haiwezekani kuwe na watu 4000 hawajaandikishwa wakati walioandikishwa ni idadi hiyo hiyo.”
Aliendelea kusema: “Othman na ACT yake anapokutana na viongozi wa Dini, Mabalozi na Wakuu Jumuiya za Kimataifa wajaribu kusema ukweli. ACT acheni kupotosha mambo kwa kutafuta huruma ya Kisiasa.”