Mbeto: ACT Wazalendo wasijifananishe na CCM

0

MCHAKATO wa mchujo wa wagombea wa Ubunge, Uwakilishi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), unachukua muda mrefu kutokana na ukubwa wa chama hicho.

Akizungumza wanahabari Zanzibar jana, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema kuna vikao vingi vinapitia majina ya watia nia.

Mbeto alitoa kauli hiyo kujibu madai ya ACT Wazalendo ambao walihoji kuchelewa kutangazwa kwa wagombea wa CCM.

Alisema, jana Julai 10, 2025 walimaliza vikao ngazi ya mkoa na leo Julai 11, ni zamu ya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu Taifa.

“Vikao havijafika mwisho, CCM chama kikubwa na hata ndio maana umeona idadi kubwa ya wanachama wamejitokeza kuchukua fomu,” alisema Mbeto.

“Makada waliojitokeza kuomba ridhaa ya chama kwenye Uwakilishi, Ubunge na Udiwani Zanzibar ni zaidi ya 2,098 wakati ACT hawazidi 300, watajifananishaje na sisi..?” alihoji Mbeto.

Mwenezi huyo alibainisha kuwa, hakuna jimbo hata moja ACT, wamejitokeza watu zaidi ya wawili na kwingine hadi mmoja wakati CCM hadi makada 12 jimbo moja hivyo ni wazi kuwa hapo kunazungumziwa vyama viwili tofauti na visivyoweza kufanana hata kidogo.

Mbeto alitanabaisha kuwa, majina matatu kwa ajili ya kura za maoni yanatarajiwa kupatikana Julai 13, mwaka huu, baada ya kukamilika vikao vya mchujo ndani ya chama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here