Mbeto: ACT kitazusha uongo, hakitashinda uchaguzi Z’bar

0

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema baada ya ACT Wazalendo kuishiwa hoja za kuwaaeleza wananchi kitazua uongo na upotoshaji, lakini hakina ubavu wa kushinda urais katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

CCM kupitia kwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, kimesisitiza ACT toka sasa hadi Oktoba mwaka huu, viongozi wake watapayuka kutokana na haiba iliyopo ya ustawi wa maendeleo yaliyoimarika Zanzibar.

Mbeto alisema, hakuna kiongozi yeyote wa ACT mwenye ubavu wa kukwamisha uamuzi wa Serikali isifikie maamuzi yake ya kuchimba mafuta kwa manufaa na maslahi ya nchi na wananchi.

Alisema, hawawezi kukwamisha mpango wa uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwasababu SMZ imeshachukua hatua zote muhimu za kuanza mradi wa uchimbaji mafuta.

Alieleza, katika Serikali ya Awamu ya Saba chini ya Rais Mstaafu Dkt. Ali Mohamed Shein, ilipitishwa Sheria Namba 6 ya Mwaka 2016 ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, wakiwemo Wawakikishi na Mawaziri toka upinzani .

Pia, aliongeza kusema Mwaka 2017 chini ya Rais Dkt. Shein, SMZ ilianzisha Shirika la Maendeleo ya Petroli Zanzibar (ZPDC) na mwaka huo huo Mamlaka ya Usimamizi na Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia( ZPRA) ikaanzishwa.

“ACT Wazalendo nilishasema kuanzia sasa kuelekea Oktoba mwaka huu viongozi wake wataropoka meneno mengi kuthibisha wana mradi wa siasa chafu. Wameishiwa maneno ya kuwaeleza wananchi na sasa wanazidi kupuuzwa” alisema Mbeto.

Akifafanua zaidi, Mbeto alisema kazi ya utafutaji Mafuta na Gesi Asilia ilianza rasmi mwaka 2017 kwa njia ya mitetemo, Angani na Baharini ambapo Kampuni ya Rak Gas ya Ras Kheimah ya Falme za Kiarabu – UAE ilianza kazi hiyo na kukamilika mwaka 2019 kwa Kitalu Namba 9 cha Pemba- Zanzibar.

Aidha, Mwaka 2019, SMZ ilisaini Mkataba wa Mgawanyo wa Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia (PSA) na Kampuni ya Rak Gas bila kuwepo mivutano, migongano wala matatizo yoyote.

Akizungumzia Kitalu cha Pemba – Zanzibar, alisema kimsingi Kitalu hicho pia kimegusa maeneo ya Mkoa wa Tanga, lakini kwa kuwa Zanzibar ni sehemu ya Tanzania, Serikali ya muungano imeachia Zanzibar.

Mbeto alimtaja aliyekuwa Waziri wa Habari toka upinzani katika awamu ya saba, Said Ali Mbarouk, aliwahi kuingia mkataba mbovu na Kampuni ya AGAPE kuhusu Ving’amuzi vya runinga na kuitia hasara kubwa SMZ.

Akimzungumzia Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Mansour Yussuf Himid, Mbeto alimtaka Mwanasiasa huyo ni vema angefunga mdomo wake, akae kimya kwani akiwa Waziri SMZ hakuwa kiongozi mzalendo.

Mbeto alisema, Mansour akiwa Waziri hakufanya lolote lililoleta manufaa hususan katika suala la Mafuta na Gesi zaidi ya kukosa nidhamu kwa viongozi wake hadi akafukuzwa Uwaziri na kuvuliwa uanachama CCM.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here