Mauaji ya halaiki ya mwisho kushuhudiwa katika historia ya binadamu

0

Na Prof. Dkt. Kudret BÜLBÜL 

KWA mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusiana na makosa ya mauaji ya halaiki, Makosa hayo yanajumuisha aina yeyote ya matendo yenye malengo ya kuangamiza na kufuta kwenye uso wa dunia sehemu au kundi lote liwe la kidini, rangi, jinsia, kabila au Taifa.

Matendo hayo yanaweza kuorodheshwa kama ifuatavyo:- Kuua wanachama wa kundi fulani; Kuwapa mateso makubwa ya kimwili na kiakili wanachama wa kundi fulani.

Mengine ni kunyang’anya sehemu ya mali au mali yote ya kundi fulani, kubadilisha kwa makusudi nyenzo za maisha za kundi fulani; kuchukua hatua za makusudi kuzuia watu wa kundi fulani wasiongezeke kwa kuzaliana, kuwanasibisha kwa nguvu watoto wa kundi fulani katika kundi jingine.

Kihalisia hakukuwa na fasili kamili ya neno mauaji ya halaiki katika vitabu mpaka pale mnamo mwaka 1948 myahudi wa kutoka Poland, Raphael Lemkin, alipoelezea mpango madhubuti wa Wajerumani wa kinazi  kuwaangamiza wayahudi.

Lemkin alikuwa mwanataaluma wa kwanza kutumia neno ‘genocide,’ linalomaanisha mauaji ya halaiki. Neno hilo la genocide ni muunganiko wa maneno mawili ‘geno’ kutoka katika lugha ya Kigiriki likimaanisha ‘halaiki’  na ‘cide’ kutoka katika lugha ya Kilatini likimaanisha ‘mauaji’.

Ingawa fasili hii ilianza kutumiwa mahususi kuelezea baadhi ya matukio yaliyokuwa kinyume na ubinadamu yaliyofanywa na baadhi ya Mataifa ya Magharibi, fasili hii inatumiwa zaidi na Mataifa ya Magharibi kuelezea matukio katika Mataifa yasiyo ya Kimagharibi.

Katika makala hii tutajaribu kukuelezea mauji ya halaiki ya Rwanda. Haya ni mauaji ya halaiki ya mwisho kushuhudiwa katika historia ya binadamu ukiacha yale ya Bosnia.

Historia ya Rwanda kimsingi haitofautiani sana na Mataifa mengine yaliyotawaliwa. Kwa mara ya kwanza ilitawaliwa na Wajerumani. Baada ya Wajerumani kupoteza vita kuu ya kwanza ya dunia Ruanda ikatwaliwa na Ubelgiji.

Hata mbinu za kuitawala Rwanda hazitofautiutiani na mbinu zilizotumika sehemu nyingine. Ilichokifanya Ubelgiji nchini Rwanda ni aina nyingine ya mtindo wa Waingereza wa ‘Tenganisha, gawanya, Ongoza’.

Ubelgiji kama yalivyokuwa yakifanya Mataifa mengine mengi ya kibeberu ili kudumisha utawala wa kikoloni, ilitumia siasa ya kuunga mkono makundi ya wachache.

Wajerumani walianzisha mkakati huu wa kuwaunga mkono kabila la Watutsi ambao ni wachache dhidi ya Wahutu walio wengi, kwa misingi kwamba mafuvu ya watutsi ni bora kuliko ya wahutu. Kwa msingi huo, wakafanikiwa kuanzisha mgogoro mkubwa baina ya makabila mawili ambayo kwa maelfu ya miaka yalikuwa yakiishi kwa amani.

Ubelgiji nayo kwa upande wake kama matokeo ya siasa hizi za ‘tenganisha, gawanya, tawala’ waliiongoza nchi hio kwa kutumia Watutsi waliokuwa wachache mpaka nchi hiyo ilipopata uhuru.

Mwaka 1961 baada ya Rwanda kupata uhuru, uongozi ukawa mikononi mwa walio wengi; kabila la Wahutu. Kuanzia miaka ya 1950 na kuendelea Ubelgiji ilianza kuwaunga mkono Wahutu.

Toka muda huo Wahutu ambao walikuwa wamekandamizwa kwa muda mrefu walipopata nafasi wakaitumia kuwafanyia Watutsi vile walivyokuwa kuwa wakiwafanyiwa wao kabla.

1994: MAUAJI YA WATU MILIONI MOJA

Mvutano na mapigano kati ya Watutsi ambao ni wachache na Wahutu ambao ni wengi uliendelea mpaka mwaka 1994. Mwaka huo rais ambaye alikuwa ni Mhutu, Habyarimana alikaa meza moja kutafuta amani na Watutsi.

Makubaliano yakafikiwa. Katika makubaliano hayo ilipitishwa kwamba Watutsi nao washirikishwe katika uongozi wa nchi na pia wawe na sauti katika masuala ya nchi. Lakini, wakati Habyarimana akisafiri kwa ndege, ndege hiyo ikatunguliwa na Rais huyo kuuawa.

Wahutu ambao walikuwa wakiwatuhumu Watutsi kwa kumuua rais wa nchi, wakaanza kufekeleza umwagaji damu wa kutisha. Ndani ya siku mia moja karibu watu Milioni Moja, wengi wao wakiwa Watutsi pamoja na wasomi wa kihutu waliuawa.

Hii inamaanisha wastani watu elfu 10 waliuawa kwa siku. Katika mauaji hayo ambayo yalibarikiwa na maafisa wa serikali pamoja na vyombo vya habari, kutokana na kukosa silaha za moto za kutosha Wahutu wenye msimamo mkali waliua mamia kwa maelfu ya watu kwa kutumia mapanga, kuwachoma moto na kuwabaka wanawake.

Vitambulisho ambavyo vilitolewa na Ubelgiji ili kuweza kuwatenganisha Wahutu na Watutsi vilirahisisha kazi ya kuwatambua na kuwaua Watutsi. Baada ya siku mia moja za mauaji ya halaiki chama cha wazalendo cha Rwanda, RPF, ambacho kiliundwa na Watutsi kiliingia mji mkuu wa Rwanda na mauaji hayo ya halaiki kufikia mwisho.

Wakati mauaji ya halaiki yakianza kulikuwa na askari 2500 wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda. Nguvu pekee ambayo ingeweza kuwalinda Watutsi dhidi ya mauaji hayo ya halaiki ilikuwa ni jeshi la amani la Umoja wa Mataifa.

Lakini, kilichofanywa na jeshi la amani la Umoja wa Mataifa haikuwa tofauti na kilichofanywa mwaka 1995, Bosnia Herzegovina au kilichofanywa Srebrenica.Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lilifikia maamuzi ya kupunguza askari wa Umoja huo kutoka 2500 mpaka kufikia 250.

Ni kama vile ilivyokuwa Srebrenica ambako kamanda wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa kutoka Uholanzi Thom Karremans aliyekuwa na kazi ya kulinda amani katika mji huo alivyo waacha watu elfu 25 aliokuwa akiwalinda pamoja na Waserbia.

KUHUSIKA KWA UFARANSA

Rais wa Rwanda Paul Kagame anazilaumu Ufaransa na Ubelgiji kwa kuhusika moja kwa moja na kufanya maandalizi ya kisiasa yaliyopelekea kutokea kwa mauaji ya halaiki. Wahanga wa mauaji hayo ya halaiki wamefungua kesi dhidi ya viongozi wa Ufaransa na Ubelgiji wa kipindi hicho katika nchi hizo.  

Kanisa Katoliki la Rwanda liliomba radhi kutokana na ushiriki wa kanisa hilo katika mauaji hayo. Baraza la Kitaifa la Rwanda dhidi ya mauaji ya halaiki, mwaka 2016 lilitoa orodha ya “Waliotenda makosa ya mauaji ya halaiki na walioshirikiana nao”.

Katika orodha hiyo walikuwamo maafisa wa ngazi za juu 22 wa Ufaransa akiwemo Mkuu wa majeshi wa wakati huo Jacques Lanxade. Maafisa wa Ufaransa wanashutumiwa kwa kuwapa silaha na mafunzo watekelezaji wa mauaji ya halaiki. Juni 23 mwaka 1994, Ufaransa, ilianzisha oparesheni maalumu ya kuanzisha eneo salama kwa ajili ya wanaokimbia machafuko, Kusini Magharibi mwa nchi.

Lakini, badala ya Ufaransa kuzuia mauaji ya halaiki ikawapatia silaha watekelezaji wa mauaji na muhimu zaidi ilikuwa ikizuia kusonga mbele kwa chama cha wazalendo cha Ruanda, RPF.

Mwandishi wa Ufaransa Saint-Exupery, anasema kwamba, Hubert Vedrine aliyekuwa Katibu Mkuu wa François Mitterrand Rais wa Ufaransa wa kipindi hicho alitoa amri ya maandishi ya kuwapa silaha Wahutu.

Rais wa zamani wa Ufaransa François Mitterrand, mwaka 1998 akifanya mahojiano na gazeti la ‘Le Figaro’ alitoa maneno ya kushtusha na kutisha, alisema “Mauaji ya halaiki katika hizo nchi si kitu cha kupewa umuhimu”

Baada ya upingwaji mkubwa kutoka jamii ya Kimataifa na makundi ya haki za binadamu, hatimaye Aprili 2019, miaka 25 baadae, Rais Macron alifanya maamuzi wa kuunda tume ya kuchunguza mauaji ya halaiki.

Tume hiyo badala kuundwa na watu wasio na upande na wataalamu wa mada husika, iliundwa na watu wanaokubalika na Ufaransa kitu ambacho kilipingwa.

Labda ni ubinadamu ndio unaotufanya tufikiri kwamba, Ubeberu haupo hivi sasa, tufikiri kwamba ubaguzi unaofanywa na watu weupe ambao niliupa jina la ‘Tarrantizm’ pamoja na unazi havipo. Ni kwa sababu tungependa matukio haya ya kikatili yakabaki katika historia.

Lakini, vyovyote vile tutakavyotaka kujisahaulisha, bado nia za kibeberu na ideolojia za mauaji zipo hii leo. Na katika kila hali zinatukumbusha mambo haya. Leo hii ukilinganisha na siku zilizopita kuna silaha na njia ambazo zinaweza kumwaga damu zaidi.

Sisi kama familia ya binadamu, tuna mwelekeo wa kuona unyama haufanywi na Mataifa ya Magharibi, Unyama na mauaji hivi sasa yamepungua ukilinganisha na hapo nyuma, na yote hayo yanatufanya kutoyaona vizuri matukio hayo na kuyapinga itakiwavyo kwa wakati.

*Mwandishi wa makala hii ni Mkuu wa kitivo cha elimu ya siasa Chuo Kikuu cha Ankara Yıldırım Beyazıt.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here