‘Matuta’ yaamua ubishi wa Messi na Mbappe

0

Na Mwandishi Wetu

KILA kona ya dunia, ubishi uliokuwa umetawala ni nani atamzidi maarifa mwenzake kati ya wachezaji wawili mahiri; Lionel Messi na Kylian Mbappe ambao wote wanahudumu kwenye klabu ya Paris Saint – Germain (PSG) ya Ufaransa.

Ubishi umekwisha baada ya Argentina kutawazwa kuwa wafalme wapya wa soka duniani, baada ya kuifunga Ufaransa penalti 4-2 kufuatia sare ya 3-3 mwishoni mwa dakika 120 katika fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Lusail Iconic, nchini Qatar.

Ilikuwa mara ya tatu katika historia kwa bingwa wa dunia kuamuliwa kupitia mikwaju ya penalti. Wafalme mara tano Brazil walitwaa ubingwa wa 1994 kwa kufunga Italia 3-2 baada ya sare ya bila kufungana. Italia nao waliifunga Ufaransa 5-3 mnamo 2006 baada ya sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa ziada.

Mwaka huu, Lionel Messi aliibeba Argentina kupitia penalti katika dakika ya 23 baada ya Ousmane Dembele kumwangusha Angel Di Maria ndani ya eneo la hatari. Di Maria alipachika wavuni bao la pili la Argentina baada ya kushirikiana vilivyo na Alexis Mac Allister katika dakika ya 36.

Hata hivyo, Kylian Mbappe alirejesha Ufaransa mchezoni kupitia penalti ya dakika ya 80, sekunde 37 kabla ya kusawazisha kupitia mchomo wa Marcos Thuram. Penalti hiyo ilisababishwa na Nicolas Otamendi kumchezea vibaya Randal Kolo kwenye eneo la hatari.

Messi alirejesha tena matumaini ya Argentina katika dakika ya 108 kabla ya Mbappe kufunga penalti ya kusawazisha dakika mbili kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa. Mbappe aliibuka mfungaji bora wa fainali za mwaka huu nchini Qatar baada ya kupachika wavuni magoli manane.

Baada ya muda wa ziada kufika tamati, Argentina walipachika wavuni penalti nne kupitia kwa Messi, Paulo Dybala, Leandro Paredes na Gonzalo Montiel.

Ufaransa walifunga mikwaju yao kupitia kwa Mbappe na Kolo Muani. Kipa matata wa Argentina, Emiliano Martinez, alipangua penalti ya Kingsley Coman huku Aurelien Djani Tchouameni akiupiga nje mkwaju wake.

Argentina sasa ni mabingwa mara tatu wa dunia. Waliwahi pia kunyanyua ufalme mnamo 1978 na 1986. Walikata tiketi ya kuelekea Qatar mwaka huu bila kupoteza mechi yoyote katika hatua za mchujo. Waliambulia nafasi ya pili katika Kombe la Dunia mnamo 1990 na 2014 baada ya kuchapwa 1-0 na Ujerumani nchini Italia na Brazil.

Argentina waliofungua Kundi C kwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Saudi Arabia, walinyanyuka upesi na kulaza Mexico na Poland 2-0 kabla ya kupiga Australia 2-1 katika raundi ya 16-bora. Walifunga Uholanzi penalti 4-3 baada ya sare ya 2-2 katika robo fainali kabla ya kuinyuka Croatia 3-0 katika nusu fainali.

Ufaransa ambao ni mabingwa mara mbili wa dunia (1998, 2018) walianza kampeni za Kundi D kwa ushindi wa 4-1 dhidi ya Australia kabla ya Tunisia kuwaduwaza 1-0 baada ya kucharaza Denmark 2-1. Aidha, waliwatoa Poland katika raundi ya 16 bora kwa 3-1 kabla ya kuimaliza Uingereza 2-1 katika robo fainali, na kisha kuwabamiza Morocco 2-0 katika hatua ya nne bora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here