Masauni aagiza waliohusika na mauaji Lindi wakamatwe

0

Na Mwandishi Wetu, MoHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata mara moja wafugaji waliohusika katika mauaji ya watu 12 Mkoani Lindi.

Masauni alitoa kauli hiyo akiwa ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi katika Vijiji vya Kikole, Kipindimbi na Zinga Kibaoni Wilayani Kilwa, Mkoani humo katika ziara yao kufuatia mgogoro wa wakulima na Wafugaji mkoani humo.

Alisema, Serikali haiwezi kukaa kimya wakati matukio hayo ya kinyama yakiendelea na haitakubali kuona mfugaji au mkulima anavunja sheria, amani, hivyo lazima sheria ifuatwe na atakayekiukwa atashughulikiwa.

“Natoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha watu wote nchi nzima walioshiriki kuua watu wengine, ikiwemo hawa walioua wakulima katika Wilaya hii ya Kilwa na Wilaya zingine za Mkoa huu wa Lindi ambazo tunakwenda kwanza wakamatwe, ninashangaa mpaka leo hakuna mtu hata mmoja aliyekamatwa, inatutia mashaka makubwa,” alisema Masauni na kuongeza;

“Kamishna upo hapa na RPC upo hapa hakikisheni hawa mnawakamata haraka ili iwe fundisho kwa watu wengine, haiwezekani mtu anaua raia kama anaua kuku, watu 12 wamekufa katika mkoa huu wa Lindi, hawa ni binadamu, leo ameua mmoja akamatwi, kesho kaua mwingime hakamtwi, na hata waliofanya uhalifu kuiba au kujeruhi nao wakamatwe.”

Aliongeza kuwa, kwa yeyote ambaye ameshiriki katika kusababisha matatizo hayo ya vifo katika kutenda makusudi au kuzembea, kwa wale ambao wanaihusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na wengine ametaka kila mtu awajibike kwa nafasi yake na kila ambaye yupo chini ya Serikali kwa ujumla wake anataka wawajibike ipasavyo.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wafugaji waliopo katika vijiji ambavyo hawaruhusiwi kuwepo, waondoke katika maeneo hayo, waende katika vijiji vilivyopangwa kwa ajili ya mifugo.

“Nawataka wafugaji kuacha tabia ya kupeleka mifugo katika mashamba ya wakulima, marufuku kupeleka mifugo yenu katika maeneo ambayo hamruhusiwi ikiwemo katika Kijiji hiki cha Kikole, lazima utaratibu ufuatwe,” alisema Ndaki.

Naye Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini, CP Awadhi Haji alisema, Jeshi la Polisi litafanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwasaka wahalifu ambao wameua watu 12 katika Mkoa huo na watakamatwa na pia amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika msako huo.

“RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) ninaagiza kuanzia sasa lete askari kuja kuendesha msako nyumba kwa nyumba, ili tunataka hawa wananchi watembee kifua mbele kwenda shambani au wapi hata kwenda porini kule,”

“Mfugaji amekamatwa ahojiwe amekujaje kama Mwenyekiti amemuagiza kamata Mwenyekiti weka ndani chukua hatua kali, tusipofanya hivyo tutakuja kujuta nchi haitawaliki kwasababu ya tamaa ya watu wachache wasiotaka kuwa waadilifu katika maeneo yao ya kazi,” alisema CP Awadhi.

Mkazi wa Kijiji cha Kikole, Pili Mneka alisema kutokana na kifo cha mkulima mwenzao katika Kijiji hicho cha Kikole, Kata ya Kikole, Wilayani Kilwa, kimewaudhunisha na wanakosa amani kwa kuwa na woga kutokana na wafugaji hao kufanya ukatili kwa mkulima mwenzao.

Waziri Masauni, Waziri Ndaki na viongozi wengine wanaendelea na ziara mkoani humo, ambapo pia wanatarajia kutembelea Wilaya za Liwale na Nachingwea katika Mkoa huo kufuatilia matukio hayo ya mauaji ambayo yanasababishwa kwa sehemu kubwa na wafugaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here