Na Albert Thomas Kawogo
TAASISI ya Marian Schools Bagamoyo imeandaa mashindano ya mbio MARIAN SCHOOLS MARATHON 2025 yatakayofanyika Bagamoyo Ijumaa, Agosti 25, 2025.
Msemaji wa Marian Schools Ohsana Mnalunde amesema, mbio hizo zitaanzia kwenye kijiji cha Zinga Samakisamaki na kumalizikia kwenye hoteli ya Stella Maris Bagamoyo mjini.
Mnalunde amesema, tayari zaidi ya washiriki 5000 wamethibitisha ushiriki wao huku idadi kubwa ya watu wa Bagamoyo ikionyesha nia ya kushirki mbio hizo.

Amesema, mgawanyo wa mbio hizo ni wa Kilomita 21, KM 10 na KM 5 ambapo idadi ya washiriki ni wanafunzi, wazazi, wafanyakazi, walimu na wakuu wa mashrika ya serikali na binafsi pamoja na wafanyakazi wao.
Naye Meneja wa Taasisi za Marian Schools Padre Valentine Bayo amewataka watu wengi kujitokeza kujisajili ili waweze kushiriki kwani kukimbia ni afya na kunasaidia kupunguza kasi ya magonjwa yasiyoyakuambukiza kama shinikizo la damu sukari na moyo.
Padre Bayo ambaye pia ni mwanzilishi wa shule za Marian amesema, watu wanaingia gharama kubwa kutibu magonjwa yatokanayo na uzito wa kupindukia lakini, kama wangejenga utamaduni wa kufanya mazoezi hasa kukimbia wangeepuka magonjwa hayo.
Mbio hizo ambazo kwa mwaka huu zinatimiza miaka mitatu sasa zimedhaminiwa na Benki ya KCB.