Mapinduzi ya Zanzibar ni alama ya ukombozi – CCM

0

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar kimesema ili kukumbuka juhudi za ASP zilizouondoa usultan, Wazanzibari wataendelea kuwaenzi wote waliojitolea kuikomboa nchi yao.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis amesema Waafrika wenyeji wa Zanzibar kabla ya mwaka 1964, waliishi chini ya ukandamizaji wa haki na kubaguliwa.

Mbeto alisema, ASP kiliwaongoza Wazanzibari bila kujali rangi zao, kabila, asili wala dini, kukataa kutawaliwa katika nchi yao.

Alisema, wananchi hao chini ya uongozi wa Rais wa ASP Hayati Mzee Abeid Amani Karume, kililazimika kufanya Mapinduzi baada ya watawala kuonekana hawako tayari kukabidhi madaraka kwa njia ya uchaguzi.

“Wazee wetu kwa kutekeleza sera, shabaha na malengo ya ASP toka uchaguzi mkuu wa kwanza mwaka 1957 kilishinda. Hata chaguzi za 1961 na 1963 licha ya ASP kushinda hakikupewa utawala,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema, Waafrika wa Zanzibar hawakuona njia mbadala ya kujitawala zaidi ya Mapinduzi yaliyoleta uhuru na mamlaka kamili Zanzibar.

“Tutawaenzi mashujaa wa Mapinduzi waliojitolea muhanga kwa ajili ya ukombozi wa ndugu zao. Kwa waliopoteza maisha yao kwa ajili ya kuikomba nchi yetu Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi,” alisema.

Pia, Mbeto alisema baada ya miaka 61 kupita, kizazi kipya cha Wazanzibari kitaendela kuyalinda na kuyaendeleza Mapinduzi hayo kwa gharama yoyote chini ya uongozi wa CCM na sera zake.

“Yote yanayotekelezwa sasa na yajayo chini ya SMZ inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi yanafuata misingi iliyowekwa na ASP. Wanaodhani watayavuruga na kuivunja misingi ya Mapinduzi hawataachwa watambe,” alisisitiza Mbeto.

Vile vile, Mwenezi huyo alisema jukumu la kuyalinda Mapinduzi ni kiapo cha utii kwa kila mzanzibari aidha awe ni mwana CCM, ACT, Chadema au chama chochote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here