Mapato ya Utalii yaongezeka nchini

0

MAPATO yatokanayo na utalii imeongezeka kutoka Dola za Kimarekani Milioni 714.59 kwa mwaka 2020 hadi kufikia Dola za Kimarekani Milioni 1,310.34 kwa mwaka 2021

Taarifa hiyo imetolewa Jijini Arusha na Mwenyekiti wa Kamati ya Ripoti ya Utafiti wa Watalii ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watalii Walioondoka nchini mwaka 2021.

Naibu Katibu Mkuu Mkomi alisema, taarifa ya utafiti huo inaonesha kuwa Tanzania inazidi kufanya vizuri katika sekta ya utalii huku mapato yatokanayo na utalii yakiongezeka mwaka hadi mwaka.

Alisema, mwaka mmoja baada ya mlipuko wa janga la UVIKO-19, idadi ya watalii iliongezeka kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi kufikia watalii 922,692 mwaka 2021 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 48.6

Amezitaja sababu zilizochangia ongezeko la watalii hapa nchini mara baada ya mlipuko wa Janga la UVIKO 19 kuwa ni jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi

Mkomi alisema, matokeo ya utafiti yanaonesha idadi kubwa ya watalii walikuja hapa nchini kwa ajili ya kutembelea hifadhi za wanyamapori na fukwe.

Utafiti huo umefanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Benki Kuu Tanzania (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Idara ya Uhamiaji, Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Shirikisho la wawekezaji katika Sekta ya Utalii Zanzibar ( ZATI)

Mkomi alisema, takwimu za utafiti huo, zimepatikana kutokana na utafiti uliofanywa katika vituo vikubwa nane vya watalii, ikiwemo viwanja vya ndege vya kimataifa pamoja na maeneo ya njia za kuingilia na kutokea watalii.

Matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa idadi kubwa ya watalii wametokea nchi ya Ufaransa ikifuatiwa na Marekani, Kenya pamoja na Zambia

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Mkomi alisema, matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku hapa nchini yaliongezeka kutoka dola za Kimarekani 152 mwaka 2020 hadi kufikia dola za Kimarekani 199 mwaka 2021

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Utalii Wizara ya Maliasili na Utalii, Richie Wandwi alisema, kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imejidhatiti kuwekeza nguvu katika utalii wa fukwe kwa vile ni aina ya utalii ambao unaonekana kupendwa na watalii wengi wanaoingia nchini.

Aliongeza kuwa, Wizara itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo baadhi ya watalii wamekutana nazo ili kuhakikisha idadi ya watalii inazidi kuongezeka na vivutio vilivyopo hapa nchini vinatangazwa kwa kasi zaidi katika Jumuia za Kimataifa.

Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa dunia ambapo idadi ya watalii duniani iliongezeka kwa takribani asilimia tano na kuchangia asilimia 6.8 ya mauzo ya nje, na kuzalisha ajira Milioni 333.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here